Mabango ya Lowassa yazua kizaazaa
MABANGO yenye picha ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, yanayoendelea
kubandikwa katika maeneo mbalimbali nchini yamezua kizaazaa, baada ya
mengine kuondolewa na wale wanaofanya kazi ya kuyaweka kutishwa na hata
kuwekwa ndani na Jeshi la Polisi.
Hali hiyo imejitokeza mkoani Iringa, ambako vijana wanaofanya kazi ya
kuweka mabango hayo waliwekwa ndani na Jeshi la Polisi na jijini Dar es
Salaam ambako bango lililokuwa limewekwa katika Soko la Kariakoo
liliondolewa saa chache tu baada ya kubandikwa na hivyo kuzua mjadala
kila kona.
Wakati wale waliokamatwa mkoani Iringa wakidaiwa kuwekwa ndani
pasipokuwa na sababu yoyote hadi pale walipotolewa na maofisa wa
Chadema, Jijini Dar es Salaam bango hilo liliondolewa na uongozi wa Soko
la Kariakoo kwa madai ya kubandikwa kimakosa.
Juzi saa 12 jioni wafanyakazi wa kampuni ya Platnum Media Co. Ltd
walifika sokoni hapo na kuanza kubandika bango hilo lililokuwa na picha
ya Lowassa, ikiambatana na maandishi yanayosomeka; ‘Edward Lowassa…Ni
wakati wa mabadiliko’.
Wakati bango hilo likibandikwa umati mkubwa ulikusanyika karibu na
eneo hilo na kuanza kushangilia, huku wengine wakiimba “Rais…rais…rais”.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Meneja wa Soko la Kariakoo,
Florens Seiya, alisema yeye ndiye aliyetoa amri ya kuondolewa kwa bango
hilo kwa kuwa soko hilo ni taasisi ya umma na hairuhusiwi kuwekwa
mabango ya kampeni.
“Ni kweli tunamfahamu aliyebandika bango hilo, ni mtu ambaye tuna
mkataba naye wa kutumia ubao huo kubandika mabango, lakini hili
lilibandikwa kimakosa bila kutushirikisha,” alisema Seiya.
Alisema katika mkataba wa soko hilo na kampuni ya Platnum Media Co.
Ltd, kifungu cha sita kinamtaka aonyeshe maudhui yaliyomo katika mabango
kabla ya kubandika, kitu ambacho yeye (Platnum) hakufanya.
“Jana (juzi) baada ya kufunga ofisi na kuondoka ndipo alipofika na
kuanza kuweka bango hilo, jambo lililofanya watu wakusanyike kwa wingi
utafikiri pana mkutano wa siasa huku wengine wakishangilia,” alisema
Seiya.
Alisema kutokana na soko hilo kuwa ni taasisi ya umma, hairuhusiwi
kuweka tangazo lolote linalohusu kampeni za kisiasa kwa kuwa wao
hawafungamani na chama chochote.
“Hebu angalia mwenyewe (huku akionyesha rekodi ya video ambayo
inaonyesha watu walivyojaa huku wakishangilia wakati bango hilo
likiwekwa) nani angeweza kuilinda amani mahali hapa,” alisema.
Aliongeza kuwa hata hivyo, wamemwandikia barua mteja wao huyo,
Platnum ajieleze kwa nini alivunja kifungu hicho kinachomtaka apeleke
maudhui kabla ya kubandika chochote.
“Kifungu cha sita cha mkataba kinasema kuwa soko la Kariakoo lina
haki ya kukataa matangazo yasiyoruhusiwa kisheria na tamaduni za nchi…
hawa Platnum tunafanya nao biashara kwa takribani miaka nane na hajawahi
kubandika chochote bila sisi kukiona,” alisema Seiya.
Mtanzania imeonyeshwa barua hiyo yenye kumbukumbu namba SKM/B/125
iliyokuwa na kichwa cha habari ‘ukiukaji wa mkataba wa matangazo’ ya
Septemba 4 mwaka huu, iliyomtaka Platnum ajieleze.
Wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa nyakati tofauti, baadhi ya
wafanyabiashara wa soko hilo walisema kuwa hizo ni njama za wana CCM kwa
kuwa watu walijaa na kushangilia sana.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Hamisi Napinda, alisema saa 12 jioni
wakati bango hilo likiwekwa, polisi walifika muda huo huo na baada ya
wao kuondoka tu wakaliondoa.
“Jana (juzi) muda mfupi baada ya kubandikwa bango la Lowassa askari
walifika na difenda mbili walipoondoka tu likabanduliwa, hii ni hujuma
wanazomfanyia,” alisema Napinda.
UKAWA KUSHITAKI
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James
Mbatia, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kufanya
siasa za uchochezi na badala yake wafanye siasa safi zinazojikita katika
hoja.
Umoja huo pia leo unatarajia kuwasilisha andiko la kisheria kwa Tume
ya Uchaguzi (NEC) ambalo litakuwa na malalamiko kuhusu matukio na hujuma
zinazoendelea katika kipindi hiki cha kampeni.
Source: MTANZANIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment