Showing posts with label teknolojia. Show all posts
Showing posts with label teknolojia. Show all posts

Programu 30 za Simu ya Android Muhimu Kuwa Nazo

programu-za-android-1
Matumizi ya simu za SmartPhone yameongezeka sana kote duniani na ikiwemo Tanzania.
Japo simu hizi zinatumika sana ,utafiti unaonyesha kuwa vitu vingi vilivyomo katika simu hizi havitumiwi ipasavyo na baadhi ya watumiaji hata hawajui hata kama simu zao zina uwezo wa kufanya mambo hayo.
SmartPhone ni simu zinazowezesha kuweka au kutoa programu za ziada kuliko zile zilizowekwa na watengenezaji kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali katika simu.
Programu nyingi sana zinatengenezwa kila siku na kuuzwa katika masoko katika mtandao(Android Market na Google Play). Baadhi ya programu hizi ni za bure na zinamuwezesha kila mwenye simu kuweza kuzitumia na kufaidika.
Android ni Programu Mama inayoendesha mfumo wa simu yako aina ya Smartphone. Programu hii imetengenezwa na kumilikiwa na Kampuni ya Google.
Kuna programu za picha,kucheza sauti na video na za kukuwezesha kusoma taarifa mbali mbali.
Hapa tunakuleteeni orodha ya programu za simu ya android 30 ambazo ni muhimu kwa yeyote mwenye simu ya android

Programu 30 Muhimu na Bure za Simu ya Android kwa Yeyote:

1. Merriam Webster

Mojawapo ya kamusi maarufu duniani ya kiingereza kwa kiingereza katika simu yako.
Programu hii inaweza pia kutafuta neno kwa sauti. Inatoa maana ya neno na mifano ya maneno yenye maana sawa(synonyms) na maana tofauti(antonyms). Inatoa mfano wa matumizi na jinsi ya kutamka.

2. MoboPlayer

Inacheza aina nyingi maarufu za video(mp4,mkv,mov na nyingine) na inakuwezesha kutafuta mafaili ya video wakati inapoanzishwa.
Si programu nyingi ambazo zinauwezo wa kufanya hivi,hivyo MoboPlayer ni programu muhimu katika simu yako.
Inauwezo wa kutengeneza orodha ya video katika maktaba yake na hivyo kurahisisha mpangilio na upatikanaji wa mafaili.

3. WebMD

Ni programu inayotoa msaada wa taarifa za kiafya na inakusaidia kufanya maamuzi.
WebMD kwa Android inasaidia kuweza kufahamu juu ya afya yako kwa kukupa taarifa za kiafya ambazo nitakufanya kuchukua hatua sahihi juu ya afya yako.
Ina huduma za kuangalia dalili za magonjwa,ushauri wa dawa na athari zake, msaada juu ya huduma ya kwanza na orodha ya vituo vya huduma ya afya karibu na wewe.

4.Pocket

Katika ulimwengu wa mtandao,utunzaji wa taarifa za siri kama taarifa za benki,barua pepe na tovuti mbalimbali ni changamoto kubwa.
Pocket inakuwezesha kutunza taarifa hizi sehemu moja na kwa usalama. Mtumiaji atatakiwa kukumbuka nenosiri kuu moja tu (master password) kwajili ya kufungua programu ya Pocket.

5. MX Player

Ni programu inayokuwezesha kucheza mafaili ya video na sauti karibu aina zote. Ni rahisi kutumia na inayoaminika.

6. Quickoffice

Inakuwezesha kurekebisha mafaili ya MS excel,word na mengine kwenye simu yako ya android.
Inakuwezesha pia kutuma na kupakua mafaili hayo kwenye hifadhi ya mtandao ya Google Drive ambayo inakuwezesha kupata mafaili yako popote kwenye mtandao wa intaneti.

7. Evernote

Inakuwezesha kuandika maneno,kurekodi sauti,kupiga picha kutumia simu yako na kutunza katika hifadhi ya intaneti na kukuwezesha kusoma mafaili hayo kupitia kompyuta au simu nyingine.
Akaunti ya bure inakuwezesha kuweka hadi kiasi cha MB 60 cha taarifa kwa mwezi. Ukitaka akaunti ya kubwa (pro) utahitaji kulipia $ 45 kwa mwaka.

8. Last.fm

Last.FM inakuwezesha kusikiliza muziki moja kwa moja toka kwenye intaneti kwenye simu yako.
Pia inakuwezesha kupangilia muziki wako katika orodha unayoipenda.

9. Instagram

Inakuwezesha kupiga picha na video na kuwatumia marafiki kupitia mtandao wa instagram

 10. Flickr

Inakuwezesha kupiga picha na kuwatumia marafiki kupitia mitandao ya jamii kama facebook na twitter.

11. Dropbox

Ni programu inayokuwezesha kutunza taarifa katika hifadhi iliyopo katika mtandao,na kukuwezesha kuzipata kupitia simu au kompyuta tofauti kokote duniani.
Inakuwezesha pia kushiriki na watu wengine ambao utawakaribisha.

 12. Amazon Kindle

Inakuwezesha kusoma vitabu vya kielectroniki katika mtandao toka Amazon-Wauzaji maarufu wa vitabu duniani.

13. Love Film By Post

Kwa wapenzi wa filamu,programu hii inakuwezesha kupangilia taarifa za filamu mbalimbali unazozipenda na kuona vidokezo vyake kupitia simu yako

14. Chrome

Programu inayokuwezesha kuangalia taarifa katika intanet toka Google. Inahitaji Android 4.0 na kuendelea.

 15. TED

Inakuwezesha kuona mazungumzo kwa njia ya video toka katika mtandao maarufu wa www.ted.com
Unaweza kupakua taarifa toka mtandao huu kwenye simu yako bure.

 16. Wikipedia

Inakuwezesha kupata taarifa toka mtandao wa wikipedia.com na kuweza kupakua taarifa katika simu yako na kusoma hata kama hakuna intaneti.

17. FaceBook Messenger

Inakuwezesha kuwasiliana moja kwa moja na marafiki walio kwenye mtandao wa FaceBook bila kuonyesha picha na taarifa nyingine zilizopo kwenye facebook.com.

18. Any.do

Inakuwezesha kupangilia kazi zako za siku na kukukumbusha muda unapofika

 19. VLC for Android Beta

Ni ingizo jipya katika soko. VLC inakuwezesha kucheza video na sauti za aina tofauti katika simu yako.

 20. Comics

Inakupa vichekesho kila siku katika simu.

 21. Viber

Inakuwezesha kutuma ujumbe wa maneno,picha na video kwa watumiaji wengine wa viber bure. Pia inakuwezesha kupiga simu kupitia mtandao wa intaneti bure.

 22. Skype

Inakuwezesha kuwasiliana na watu wengine kupitia mtandao wa intaneti kwa maneno,sauti na video bure.
Pia unaweza kupiga simu yoyote ya mezani na mkononi duniani kote kwa gharama ndogo sana.

23. AppLock

Programu hii inafunga programu nyingine katika simu yako kama sms,majina ya watu katika simu,programu za barua pepe,facebook,programu ya picha na nyinginezo kwa ajili ya kutunza siri zako katika simu.
Usiogope tena kumpa simu rafiki au mtoto, AppLock inakupa uhuru.

 24. Docs To Go 4.0

Inakuwezesha kutunza na kusoma mafaili ya aina tofauti (kama MS Word,PDF n.k) katika simu yako na inakuwezesha kutunza katika hifadhi za mtandaoni.

 25. Mobile Doc Scanner

Ni programu inayokuwezesha kupiga picha taarifa zilizomo katika karatasi au picha na kuziweka katika mfumo wa PDF na kuweza kuzituma kwenye mtandao kupitia barua pepe au hifadhi za mtandaoni.

26. Google Translate

Inakuwezesha kutafsiri maneno toka katika lugha moja kwenda nyingine kutumia simu yako hata bila kuwa na intaneti.
Ina uwezo wa kutafsiri lugha 80

27. Google Goggles

Inauwezo wa kusoma picha na michoro na kutafuta taarifa zake katika mtandao wa google.com
Inauwezo wa kusoma barcode ,QR Code na OCR code na kutafuta taarifa zake katika mtandao.

 28. Google Maps Navigation

Inakuwezesha kuona ramani ya dunia na eneo ulilopo.
Inakuonesha longitudo na latitudo za maeneo mbalimbali likiwemo lile ulilopo. Unaweza kuweka alama katika ramani za sehemu ulizowaji kutembelea.
Pia ina uwezo wa kukupa muelekeo wa njia kama unasafiri au ukiwa umepotea.

 29. Clean Master Phone Boost

Inakusaidia kusafisha simu yako ya Android inapokuwa nzito.
Inaongeza kumbukumbu(RAM na cache) na kuboresha spidi.
Inapunguza joto la simu kwa kusimamisha baadhi ya programu zisizohitajika.

 30. ESPN SportsCenter

Inakupa taarifa mbalimbali za michezo toka kote duniani. Matokeo ya mechi zinazochezwa katika maneno na video.

Orodha ni ndefu na hapa tumetaja chache tu. Je,unaaina nyingine za programu za simu ya android ambazo unatumia na ni nzuri? Tuandikie hapa chini katika sanduku la maoni.
Furahia matumizi ya simu yako. Jaribu programu hizi na ufaidike.

Umuhimu na Jinsi ya Kutunza Majina na Namba za Simu Kwenye Kompyuta

Imekuwa ni tatizo kwa wengi kupoteza kumbukumbu muhimu katika simu kama vile anuani na majina ya watu katika simu za mkononi.
Utasikia mtu akisema kwenye simu “wewe nani? Sina namba yako kwa sababu simu yangu ilipotea na nikapoteza namba zote”.
Ukweli ni kwamba simu nyingi za kisasa zinauwezo wa kutunza namba za simu kwenye kompyuta  pamoja na taarifa nyingine kama picha,muziki na sms kama faili ambazo unaweza ukazisoma kupitia kompyuta; au ukarudishia kwenye simu pale unapopoteza simu au kufuta taarifa kwenye simu yako.

Njia ya Kwanza: Kutumia Bluetooth
mawasiliano-simu-kompyuta
Bluetooth ni teknolojia ya kuunganisha vifaa viwili vya kielectroniki kuwasiliana na kutuma na kupokea taarifa. Inaweza ikawa mafaili ya muziki,picha,video na hata namba za zimu au anuani.
Mawasiliano yanaweza kuwa kati ya kompyuta na simu au simu na simu.
Unaweza kutumia njia hii kutuma namba za simu na anuani toka kwenye simu yako na kuhifadhi kwenye kompyuta na ukaweza kurudisha tena katika simu yoyote nyingine toka kwenye kompyuta.
Sharti ni kuwa vifaa vyote viwili vinatakiwa kuwa na teknologia hiyo ya bluetooth

Njia ya Pili: Kutumia Waya Maalumu wa USB
bluetooth-connection-phone-pc
Waya wa USB unaweza kuunganisha simu yako ili kuwasiliana na kompyuta. Kwa kutumia program maalumu ambazo simu nyingi huja nazo utaweza kuunganisha kompyuta yako na simu. Programu hizi zinakuwezesha kufanya mambo mengi kama vile unavyoweza kufanya kwenye simu ila sasa kwa kutumia kompyuta.
Mfano unaweza kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na hata kupiga simu na kuongea kama kompyuta yako ina mic na spika.
Kwa kutumia programu za aina hii unaweza ukapakua majina na hata taarifa nyingine kama  SMS na picha toka kwenye simu na kuweka kwenye kompyuta na kurudisha tena kwenye simu pale inapohitajika.

Njia ya Tatu: Kutunza Taarifa Kwenye Hifadhi ya Intaneti
cloudstore-connection-phone
Ukiwa na simu aina ya Smartphone na umeunganishwa kwenye mtandao wa intaneti,unaweza ukahifadhi kumbukumbu za simu yako ikiwemo majina na namba za simu kwenye hifadhi za intaneti (“Cloud Storage”) mfano wa huduma hizo ni ile inayotolewa na Google iitwayo Google Drive , Dropbox ,skydrive (Sasa inaitwa OneDrive) na nyingine nyingi.
Unaweza ukajiunga moja kwa moja toka kwenye simu au kutumia kompyuta.
Kama unatumia kompyuta unaweza ukajiunga na huduma hizi na kutumia kama diski ya kawaida katika kompyuta yako.

Njia ya Nne: Kupakua kwenye Kadi ya Kumbukumbu ya Simu (Memory Card)
sd-card-storage
Unaweza ukahamisha majina yote kwenda kwenye faili katika kadi ya simu.
Kisha ukahamisha faili toka kwenye kadi ya simu kwenda kwenye kompyuta kutumia blutooth au waya wa USB.
Pia unaweza ukahamisha kwa kutoa kadi na kuitunza nje ya simu (Njia hii haihitaji kuwa na kompyuta).

Kwa jinsi hii basi hutapata shida kwa kupoteza taarifa zako katika simu kwani utaweza ukarudisha taarifa zote pale unapopoteza simu na kununua simu mpya au pale unapobadirisha simu.
Unaweza ukafanya mwenyewe kama ni mjuzi wa kutumia simu na kompyuta, vinginevyo omba msaada wa kitaalamu toka kwa mtu anayefahamu. Wataalamu wa TEHAMA wanaweza kukupa msaada mzuri zaidi.
Kumbuka kuwa mbinu hizi ni baadhi ya simu tu ambazo zina uwezo mkubwa au “Smartphone”.

Mfumo wa Umeme Jua Unavyofanya Kazi na Matumizi Yake



solar-panel-2
Tunaweza kubadili mwanga wa jua moja kwa moja kuwa umeme kwa kutumia seli ya jua.
Mwanga wa jua unapopiga Paneli za Jua kwa chembe za miali yake zinazojulikana kama fotoni (Kwa kiingereza photons),panaeli za jua hubadili fotoni hizo kuwa electroni zinazofanya mkondo mnyoofu wa umeme-aina hii ya umeme inaitwa Umeme Jua.
Electroni hizi hutoka katika paneli na kuingia katika kifaa kiitwacho Inveta ambacho huubadili kuwa mkondo geu wa umeme.
Huu ni umeme ambao hutumika na vifaa vingi vya majumbani kama pasi,taa ,redio na TV.

Seli za Jua

Seli za nishati ya jua zinaundwa na paneli za umbo mraba zilizotengenezwa na madini ya silikoni na mengine yenye kupitisha umeme.
Mwanga wa jua unapopiga seli hizi,athari za kikemikali husababisha elektoni kutoka na kuzakisha mkondo wa umeme.
Seli hizi zinaitwa kitaalamu “Photovoltaic Cells” au “PV Cells” ambazo hutumika pia katika vifaa kama mashine za hesabu,saa au kompyuta ndogo.
umeme-jua_seli
Athari hizi za umeme jua ziligunguliwa kwa mara ya kwanza na mwanafizikia wa Kifaransa, Edmund Bequerel, mwaka 1839, ambaye aligundua kuwa baadhi ya metali zilikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme zikipigwa na mwanga. Uvumbuzi huu ndio unaotumika katika utengenezaji wa seli za jua.

Vifaa Vinavyofanya Mfumo wa Nishati ya Jua

Mfumo wa umeme jua hujumuisha vitu vifuatavyo:
  1. Moduli:Makundi ya seli kadhaa ambayo kwa kawaida inaitwa paneli: Huzalisha umeme wakati miali ya jua inapogonga katika uso wa seli.
    umeme-jua_paneli
  2. Betri (moja au zaidi): Hutunza umeme ambao hutumika wakati jua halipo na moduli haziwezi kuzalisha umemeumeme-jua_betri
  3. Kidhibiti chaji(Charge Regulator/Controller): Huzuia moduli kuchaji betri kupita kiasi na kuziharibuumeme-jua_kidhibiti-chaji
  4. Inveta-Hubadili nishati ya jua kutoka mkongo myoofu(DC) kwenda mkondo geu(AC).umeme-jua_inveta

Matumizi ya Mfumo wa Umeme Jua katika Biashara na Nyumbani

Mfumo huu unaweza kutumika nyumbani au sehemu ya biashara kiurahisi sana kwa ajili ya kuwasha taa au vifaa vingine vinavyotumia umeme kama redio na TV.
Paneli za jua zinaweza kujengewa katika paa la nyumba au kujengewa chini.
Kwa kawaida paneli huwekwa kwa kuelekezwa upande wa kusini.
Mfumo ungine ni ule wa kuweka vingamuzi ambavyo huelekeza paneli upande ambao jua liko. Mfumo huu ni bora zaidi kwani hupata mwanga wa jua kwa muda mrefu.
Paneli za jua zinahitaji kupata mionzi ya jua moja kwa moja na hivyo inashauriwa kuwekwa sehemu amabyo haitazibwa na kivuli chochote.
paneli_msimiko
Paneli ya Kusimama
paneli_paa
Paneli ya Juu ya Paa

Ukubwa wa Mfumo wa Nishati Jua

Ukubwa wa mfumo wa nishati ya jua unategemea vitu kadhaa ikiwemo kiasi cha umeme unachohitaji kulingana na vifaa unavyotumia,ukubwa wa paa lako(kama unatumia paa la nyumba) na kiasi cha fedha ambacho uko tayari kutumia kwani vifaa hivi vinahitaji pesa.
Ukiwa na paneli nyingi zaidi zenye uwezo mkubwa utapata umeme mkubwa zaidi na hivyo gharama itakuwa kubwa.
Na ukiongeza paneli utahitaji betri zaidi za kutunza umeme.

Teknolojia Nyingine Za Jua

  1.  Mfumo wa Maji Moto:Mfumo wa kuchemsha maji ambapo paneli maalumu zinzowekwa kuelekea jua hukusanya joto la jua na kuchemsha maji.
  2. Majiko ya Kupikia:Mabati maalumu au vioo vilivyokunjwa hutumika kukusanya joto sehemu moja na kutumika kupikia vyakula
  3. Magari au Mitambo ya Jua:Kuna mitambo inayoendeshwa kwa kutumia umeme wa jua. Mfano magari,boti na treni.

Faida za Umeme Jua

Hizi ni sababu kubwa za kuchagua kutumia nishati ya umeme-jua:
  1. Rafiki wa Mazingira
    Ni mfumo wa nishati mbadala ambayo haitoi moshi kwasababu haina vitu vinvyotembea na hivyo kutoharibu hewa kwa hewa ya ukaa kama nishati nyingine
  2. Kupunguza Bili ya Umeme
    Bili ya umeme itashuka kama ukitumia umeme wa jua. Baadhi ya vifaa kama taa na redio mfano vinaweza kutumia umeme wa jua na vitu kama jiko na pasi pekee vikatumia umeme wa gridi.
  3. Kiwango kidogo cha matengenezo
    Kwa kuwa hakuna vitu vinavyotembea hivyo mfumo huu hutumika muda mrefu sana bila kuhitaji matengenezo yoyote. Watengenezaji wengine hutoa waranti ya hadi miaka 25
  4. Ufanisi
    Bila kujali wapi unaishi jua linapatikana na umeme wa jua ni suluhisho kwa wale wanaokaa mbali na miundo mbinu ya umeme. Vijiji vingi vya Asia na Afrika vinahitaji umeme wa aina hii.

Hasara za Umeme Jua

  1. Utegemezi wa jua
    Hasara kubwa ya umeme wa jua ni kuwa inategemea jua na kama jua lisipowaka  kwa siku kadhaa basi utakosa nishati
  2. Nguvu ndogo
    Umeme wa jua hauna uwezo wa kuendesha vifaa vinavyohitaji umeme mkubwa kama vile pasi na majiko hivyo uhitaji wa mfumo ungine wenye kutoa umeme mkubwa.
Nishati jua ni technolojia ambayo ni rahisi kuendesha japo inahitaji fedha nyingi kidogo mwanzoni kwaajili ya vifaa. Inatoa mbadala katika mfumo wa kawaida wa umeme ambao gharama zake zinapanda kila siku. Umeme wa jua huenda ukawa ni upande wa kukimbilia ili kupunguza matumizi ya fedha katika nishati ya umeme.
Pia kwa vijijini ni fursa ya kuleta maendeleo ya kiteknolojia,TV na simu vinawezekana sasa hata ukiwa vijiji vya mbali ambako umeme wa kawaida haujafika. Umeme jua unaweza kuleta mapinduzi makubwa kimaendeleo Afrika

 

LIKE PAGE YETU UWE WA KWANZA KUPATA HABARI MPYA. Just Click Like Button Below...

Powered By OnlineBlogger