Inasemwa kuwa kuwa tajiri haihusiani na kiasi gani unapata bali ni kiasi gani unabakiza baada ya matumizi.
Haijarishi unapata kiasi gani cha fedha,swali linabaki unaokoa kiasi
gani. Kama wote mnabakiwa na salio la sifuri basi wote ni masikini.
Kanuni rahisi ya mahesabu inasema hivi:
Salio= Mapato-Matumizi
Hii ina maana kuwa ili ubaki na salio kubwa nia aidha ufanye hivyo kwa kuongeze kipato au kwa kupunguza matumizi ya fedha.
Kuongeza kipato ni njia bora zaidi japo wakati mwingine si rahisi sana na unabakiwa na chaguo moja tu la kupunguza matumizi ya fedha.
Cha msingi hapa ni kuwa kuna mahitaji ya muhimu kwa binadamu yeyote
kama chakula,malazi na mavazi na yale mengine ya maendeleo muhimu kama
elimu,ujenzi na michango ya kijamii ambayo ni ya lazima.
Utofauti mara nyingi unakuja kwenye kiasi cha kila kimoja katika hayo matumizi.
Wakati baadhi ya familia mfano ya watu 4 wanahitaji mlo wa sh 5,000
kwa siku familia nyingine yenye ukubwa sawa huenda ikatumia sh 30,000
kwa siku.
Ninachotaka kusema hapa ni kuwa mara nyingi matumizi makubwa ya fedha
binafsi au ndani ya familia yanaenda katika vitu visivyo vya muhimu
sana kama tutakavyoona hapa chini.
Zifuatavyo ni namna tofauti za kupunguza matumizi ya fedha yasiyo ya lazima:
#1: Tengeneza Bajeti ya Matumizi na Uifuate
Panga bajeti ya matumizi ya fedha zako. Hii itakusaidi kuona vitu gani ni muhimu kuvifanya na vipi si muhimu.Bajeti yako iangalie malengo yako ya muda mfupi na muda mrefu.
Mfano kama ulipanga kuanza ujenzi wa nyumba yako mwaka huu na umepanga kuweka akiba benki kwa ajili ya ujenzi basi hakikisha unaweka hilo katika bajeti ya kila mwezi.
Usipofanya hivyo utajikuta unatumia fedha hivyo kunywa bia au kitu kingine kisicho na kipaumbele sana na wala hakipo katika malengo uliyojiwekea.
Hivyo bajeti inakupa adabu juu ya matumizi yafedha uliyoihangaikia sana.
#2: Kata Matumizi yasiyo ya Lazima
Ukishaandaa bajeti pitia na kata matumizi yote yasiyolete matokeo katika malengo yako ya mwaka au miaka 5.Hayo si matumizi ya lazima na sio kipaumbele angalau katika mwaka huu.
#3: Punguza Safari Unazotumia Gari lako Binafsi
Mojawapo ya matumizi makubwa ya familia nyingi ni katika usafiri hasa kama unatumia usafiri binafsi.Hebu fikiria na hesabu ni kiasi gani cha mafuta unatumia kwa siku? Piga hesabu ya mwezi na ikiwezekana kwa mwaka. Utashangazwa na kiasi cha fedha unatumia katika gari pekeyake.
Tumia usafiri wa jumuia kwa baadhi ya safari. Kwanza ni vizuri kwa kutengeneza ujamaa na watu. Utaonana na watu wengi unaowafahamu katika usafiri wa jumla kuliko usafiri binafsi.
Tembea kama unakokwenda ni karibu, ninzuri kwa afya pia lakini mwishowe utapunguza matumizi ya fedha kwa kiasi kikubwa sana.
#4: Nunua Vitu kwa Jumla Badala ya Rejareja
Bei ya vitu iko chini ukinunua kwa jumla kuliko rejareja.Manunuzi ya vitu kama vyakula na mahitaji mengine ya nyumbani kama sabuni na hata mavazi ni rahisi zaidi kwa jumla kuliko kimoja kimoja,au ukinunua kidogo kidogo.
Vitu kama mchele,sukari,sabuni za kufulia,maharage na kundekunde ni bora zaidi vikinunuliwa kwa jumla na utapunguza matumizi kwa kiasi kikubwa.
#5: Azima baadhi ya Vitu Badala ya Kununua
Mojawapo ya njia maarufu ya kupunguza matumizi inasema “Kama unaweza kuazima basi usinunue”.Kuna vitu ambavyo unatumia mara chache au mara moja tu,ni vyema ukaazima badala ya kuvinunua.
Mfano DVD za sinema, au michezo ya kuigiza,mkasi wa maua vinaweza vikaazimwa toka kwa maduka yanayoazimisha au hata kwa jirani.
Kuazima kitu toka kwa jirani inaongeza ushirikiano wa kijamii ambacho ni kitu kizuri.
#6: Fanya Baadhi ya Kazi za Nyumbani Mwenyewe
Unaweza kupunguza matumizi ya fedha nyumbani kwa kufanya badhi ya kazi mwenyewe badala ya kuajiri mtu.Badala ya kuaajirimtu kukata majani ya mifugo mmoja wa familia anaweza akafanya hilo.
Kutengeneza na kumwagia maji bustani ya maua ni kazi nyingine ambayo haihitaji kuajiri mtu kuifanya na inakupa faida ya kufanya kazi ya kushughulisha mwili,yaani mazoezi ya mwili ambayo ni muhimu kwa afya njema.
#7: Punguza Kula Chakula Nje ya Nyumbani
Vyakula vya mikahawani ni ghari kuliko nyumbani.Kula nje ya nyumbani ni kitu kizuri kwa familia lakini ni vyema kama kitafanyika kwa kiasi kidogo.
Badala ya kutoka kila wiki jioni basi mnweza mkafanya mara moja kwa mwezi au isizidi mara mbili.
#8: Kopa Mikopo yenye Riba Nafuu na Lipa kwa Haraka
Watu wengi wanafanya makosa sana kipengele hiki, wanakopa toka benk au mashirika ya mikopo bila kuangalia madhara ya riba na muda wa kurejesha mkopo.Chagua mikopo ya riba nafuu na pia weka kipindi kifupi kuresha mkopo. Unapokaa na mkopo kwa muda mrefu unalipa riba kubwa zaidi.
#9: Punguza Matumizi ya ATM
Mashine za kutolea fedha za benki(ATM) zinatoza ada kila mara unapotoa fedha.Watu wanafikiri si fedha nyingi lakini kama ukipiga mahesabu utagundua si fedha ya kubeza.
Hesabu ni marangapi unatoa fedha benki kupitia ATM kwa mwezi na zidisha kwa gharama kwa kila mwamala unaofanya.
Panga ni mara ngapi unatoa fedha benki na usitoe kidogo kidogo,toa kwa mkupuo.
Kuna watu wakitaka kutoa laki 4 (400,000) wantoa laki moja moja mara nne,wakati angweza kutoa mara moja;ni hasara kubwa.
#10: Punguza au acha Matumizi ya Pombe
Pombe ni sehemu nyingine ambayo fedha hufukiwa. Wanywaji wa pombe hutumia fedha nyingi sana kwa kunywa wao binafsi na kwa kuwanunulia watu wengine.Lakini matumizi hayaishii kwenye pombe peke yake bali hununua vyakula ambavyo vingi ni hatarishi kwa afya kama nyama na vyakula vingine ambavyo huliwa kwa kiasi kikubwa kuliko inavyohitajika.
Inasemekana pia ulevi wa pombe huenda unapelekea kushawishi kudhubutu kufanya ngono hatarishi.
Kuacha kunywa pombe au kupunguza idadi ya vyupa unavyokunywa kutakusaidia kupunguza matumizi ya fedha kwa kiasi kikubwa.
Chukua Hatua Sasa…
Kuna mambo mengine mengi ambayo yanaweza kukusaidia kupunguza matumizi ya fedha na haya ni yale machache tu. Je unalo jingine? Tuandikie katika sanduku la maoni hapo chiniKama una nia ya dhati ya kupunguza matumizi ya fedha basi utayafanyia kazi,hata kama si yote basi chagua yale ambayo unaweza kuyafanya kwa ufanisi na fuatilia kujua ni kiasi gani umeokoa kwa kubadilisha tabia ya matumizi yako.
Kumbuka kuwa “Kila shilingi unayookoa ni sawa na shilingi uliyoivuna”.
Anza leo na ufaidike binafsi na familia yako.
Nawatakia mabadiliko mema!
0 comments:
Post a Comment