Matatizo Madogo ya Ujauzito

Utangulizi

Katika ujauzito, mwili wa mwanamke hubadilika kwa njia nyingi – jinsi ulivyojifunza katika Kipindi cha 7. Matatizo haya yanaweza kumkosesha utulivu. Hata hivyo, mara nyingi huwa ya kawaida. Yanaweza kutokea wakati wowote katika ujauzito. Katika kipindi hiki, utajifunza kuhusu baadhi ya matatizo madogo ya ujauzito na ujadili njia za kuwasaidia wanawake kujihisi vyema au angalau waache kuwa na hofu kuyahusu. Pia tutaeleza jinsi ya kutambua ukosefu wa utulivu kwa mwanamke unapoashiria kuwa huenda kukawa na tatizo linalohitaji uchunguzi zaidi na udhibiti, au hata kuwa jambohatari linatendeka kwa ujauzito wake. Mengi ya matatizo haya madogo katika ujauzito yanaweza kupunguzwa kwa elimu bora na matibabu ya mara moja. Pia unapaswa kujua kuhusu baadhi ya tiba zilizo hatari kwa wanawake wajawazito na zinazoweza kumdhuru mtoto.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 12

12.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyochapishwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 12.1)
12.2 Kutambua matatizo madogo yanayoweza kuwakumba wanawake katika ujauzito na ueleze jinsi yanavyoweza kudhibitiwa. (Maswali ya Kujitathmini 12.2 na 12.3)

12.1 Matatizo yanayohusiana na mmeng’enyo wa chakula na chakula

Kuna matatizo kadhaa yanayotokea sana yanayohusiana na chakula, au umeng’enyaji wa chakula. Njia nyingine ya kuyaainisha matatizo haya ni kuyachukulia kama yanayoathiri mfumo wa ufereji wa utumbo.

12.1.1 Kichefuchefu, kutapika, na hiparemesisi gravidaramu

Wanawake wengi hupata kichefuchefu na kutapika katika trimesta ya kwanza (miezi 3) ya ujauzito ambayo mara nyingi huitwa kigegezi cha asubuhi. Hutokea sana asubuhi mwanamke anapotoka kitandani. Utoaji mate kupindukia ni tatizo lisilotokea sana bali linalokera mno na linalohusiana na hali iitwayo hiparemesisi gravidaramu – inayosababishwa na kichefuchefu kikali cha mara kwa mara na kutapika kupindukia katika ujauzito.
Hiparemesisi humaanisha ‘kutapika kupindukia’. Gravidaramu humaanisha ‘katika ujauzito’.

Hiparemesisi gravidaramu ni tatizo kali kiasi kwamba mwanamke aliye nalo anapaswa kulazwa hospitalini au katika kituo cha afya.
Utambuzi wa hiparemesisi gravidaramu hufanywa mwanamke akipoteza kilo 5 au zaidi za uzani wa mwili wake kutokana na kutapika mara kwa mara, kupoteza viowevu vya mwili na kichefuchefu, na hali hii humfanya aogope kula, na huthibitishwa kwa kuwepo kwa kemikali za asidi (ketoni) katika mkojo wake. Mwili huanza kutoa ketoni unapoanza kusaga protini kwenye misuli kutokana na ukosefu wa chanzo mbadala cha nguvu ili kumweka mtu hai. Ketoni hizo zinaweza kugunduliwa kwenye mkojo kwa kipimo cha dipstick unachoweza kumfanyia mwanamke nyumbani kwake au katika Kituo cha Afya iwapo umepewa dipstick zifaazo na kuonyeshwa jinsi ya kuchunguza na kutambua mabadiliko ya rangi iwapo ketoni zimo.Matokea chanya ya kipimo hiki humaanisha kuwa sharti apewe rufaa mara moja ili aweze kupata lishe, viowevu vya mwili na kemikali muhimu mbadala, na apate matibabu ya kumkinga ili asije akakumbwa na matatizo haya tena.
Udhibiti wa kichefuchefu kisicho kikali
Ikiwa kichefuchefu si kikali, mhimize mwanamke kujaribu moja ya tatuzi hizi:
  • Kabla ya kulala au usiku, kula chakula kilicho na protini, kama vile maharagwe, njugu au jibini.
  • Kula ndizi chache, mkate mkavu, kita kavu, au vyakula vingine vya mbegu anapoamka asubuhi.
  • Kula milo mingi midogo badala ya milo miwili au mitatu mikubwa, na kunywa kiasi kidogo cha viowevu mara kwa mara.
  • Kunywa kikombe cha mnanaa, mdalasini au chai ya tangawizi mara mbili au tatu kwa siku kabla ya kula. Weka kijiko kimoja cha chai cha mnanaa, au kijiti cha mdalasani kwenye kikombe cha maji moto kisha ungoje kwa dakika chache kabla ya kunywa. Kutengeneza chai ya tangawizi, chemsha mzizi wa tangawizi uliokatwa vipande au kupondwa kwa angalau dakika 15.

12.1.2 Kutopenda chakula na tamaa ya chakula

Huenda mwanamke mjamzito akachukia kighafla chakula alichopenda hapo awali. Ni SAWA kutokula chakula hicho, na huenda akaanza kukipenda tena baada ya kuzaa. Anafaa kuwa makini kuhakikisha kuwa lishe yake ina vyakula vyenye virutubishi vingi. Utajifunza ushauri wa kumpa mwanamke kuhusu lishe bora katika ujauzito katika Kipindi cha 14.
Tamaa ya chakula (pia hujulikana kama pika) ni hamu kubwa ya kula aina fulani ya chakula, au hata kitu ambacho si chakula kama vile udongo mweusi, chaki au mchanga (Mchoro 12.1). Mwanamke akipata tamaa ya vyakula vyenye virutubishi (kama maharagwe, mayai, matunda au mboga), ni VYEMA kwake kula kiasi anachotaka.
Mchoro 12.1  Tamaa ya chakula ni kawaida mwanzoni mwa ujauzito.
Mwanamke aliye na tamaa ya kula vitu visivyo chakula kama vile udongo au mchanga anafaa kushauriwa asivile. Vinaweza kumsumisha yeye na mtoto wake. Pia vinaweza kumpa vimelea kama minyoo, vinavyoweza kumfanya awe mgonjwa. Badala yake mhimize ale vyakula vyenye ayoni na kalisi (tazama ushauri katika Mchoro 12.1).

12.1.3  Kiungulia

Hisia ya mchomo au maumivu tumboni au kati ya matiti, huitwa kutomeng’enyeka au kiungulia. Kiungulia hutokea kwa sababu mtoto anayekua hujaza fumbatio la mama na kusukuma tumbo juu zaidi ya kawaida (Mchoro 12.2). Asidi zilizo kwenye tumbo la mama zinazosaidia katika umeng'enyaji wa chakula husukumwa juu kwenye kifua chake ambapo husababisha hisia ya mchomo. Mhakikishie kuwa hii si hatari na huisha baada ya kuzaa.
Mchoro 12.2  Kiungulia katika ujauzito kinaweza kutokana na mtoto kujaa kwenye fumbatio la mama.
Udhibiti
Hapa kuna mambo ambayo mwanamke anaweza kufanya ili kuhisi utulivu zaidi:
  • Kutojaza tumbo yake kwa kula milo midogo midogo mara kwa mara, na kwa kula vyakula na kunywa viowevu vikiwa kando.
  • Kuepuka vyakula vyenye viungo au mafuta, kutumia kahawa, au kuvuta sigara kwa sababu hivi vyote vinaweza kusababisha mchomo tumboni.
  • Kula papaya au nanasi mara kwa mara kwa sababu matunda haya yana enzaimu (kemikali maalum) zinazosaidia tumbo kumeng'enya chakula.
  • Kuweka kichwa chake juu zaidi ya tumbo anapolala au kupumzika. Hii itasaidia kudumisha asidi za tumbo kwenye tumbo na si kifuani.
  • Kutuliza asidi tumboni kwa kunywa maziwa, au dawa za kudhibiti asidi zenye kiwango cha chini cha chumvi (kiowevu au tembe zinazotuliza tumbo) zilizo na asprin, lakini mshauri ajaribu kutumia mbinu zingine kabla ya kutumia dawa kama za kudhibiti asidi.

12.1.4  Uyabisi wa utumbo

Wanawake wengine wajawazito huwa na ugumu wa kupitisha kinyesi. Hii huitwa uyabisi wa utumbo. Husababishwa na mabadiliko katika homoni ambayo hupunguza mienendo ya misuli ya utumbo (usukumaji wa chakula chini kwenye koromeo), inayosukuma chakula kwenye matumbo. Hii husababisha ongezeko katika ‘muda wa kuondoa’, muda wa kumeng'enywa kwa chakula na uchafu unaondolewa kama kinyesi.
Udhibiti
Kuzuia au kutibu uyabisi wa utumbo, mwanamke mjamzito anapaswa:
  • Kula matunda na mboga kwa wingi.
  • Kula nafaka nzima (wali wa rangi ya kahawia na ngano, badala ya wali au unga mweupe).
  • Kunywa angalau vikombe vinane vya maji kwa siku.
  • Kutembea na kufanya mazoezi kila siku.
  • Jaribu tiba za nyumbani au mimea ambazo zitalainisha kinyesi au kukifanya kiwe telezi, kwa mfano, tiba zinazotokana na mbegu za telba, matunda fulani, au mimea yenye nyuzi kama vile gomeni.

12.2 Vena zilizovimba

Kuna sababu nyingi za kuvimba kwa vena za wanawake wajawazito katika sehemu tofauti za mwili. Hizi ndizo sababu mbili kuu.

12.2.1  Uvarikosi (vena varikosi)

Uvarikosi wa viungo vya uzazi unaweza kusababisha kuvuja damu ukipasuka wakati wa kuzaa, kwa hivyo, mpe mwanamke aliye na tatizo hili rufaa aende katika kituo cha afya.
Vena zilizovimba za buluu zinazotokea kwa miguu huitwa uvarikosi, au vena varikosi, na hutokea sana katika ujauzito. Wakati mwingine, vena hizi huuma. Shinikizo kutoka kwa uterasi inayokua, kwa vena zinazorudisha damu kwenye moyo kutoka kwenye miguu ni kisababishi kikubwa cha uvarikosi kwa vena za miguu. Ni nadra sana kwa vena za jenitalia za nje kuvimba, lakini zikivimba huuma sana.
Udhibiti
Ikiwa vena zilizovimba ni za miguu, zinaweza kutulia mwanamke akiweka miguu yake juu mara kwa mara. Stoki thabiti au bendeji nyumbufu pia huweza kusaidia. Ikiwa vena zilizovimba zipo karibu na jenitalia, chupi maalum ya kushikilia au padi ya usafi inaweza kumsaidia kwa kushikilia.

12.2.2  Hemoroidi

Hemoroidi ni vena zilizovimba kwenye eneo karibu na mkundu. Zinaweza kuchoma, kuuma au kuwasha. Wakati mwingine huvuja damu mwanamke anapopitisha kinyesi, hasa ikiwa ana uyabisi wa utumbo. Kuketi au kusimama kwa muda mrefu kunaweza kuendeleza athari za hemoroidi.
Udhibiti
Mwanamke anafaa kujaribu kuepuka uyabisi wa utumbo kwa kula matunda, mboga kwa wingi na kunywa maji mengi. Kulazimisha kupitisha kinyesi huendeleza athari za hemoroidi. Kuketi kwenye maji baridi au kulala chini husaidia.

12.3  Maumivu

12.3.1  Maumivu ya mgongo

Wanawake wengi wajawazito hukumbwa na maumivu ya mgongo. Uzani wa mtoto, uterasi na kiowevu cha amnioni hubadili mkao wake na kuweka mkazo kwenye mifupa na misuli ya mwanamke huyo. Kusimama mahali pamoja kwa muda mrefu, kuinama au kazi nyingi za sulubu, zinaweza kusababisha maumivu ya mgongo. Aina nyingi za maumivu ya mgongo ni kawaida katika ujauzito lakini pia zinaweza kusababishwa na maambukizi ya figo.
Udhibiti
Mhimize mume, watoto, jamaa wengine au marafiki wa mwanamke huyu kuusinga mgongo wake. Kitambaa chenye joto au chupa yenye maji moto kwenye mgongo wake pia vinaweza kumtuliza. Pia jamaa zake wanaweza kusaidia kwa kufanya baadhi ya kazi nzito kama vile kubeba watoto wadogo, kufua, kulima, na kusaga nafaka. Chupi inayokaza, au mshipi unaovaliwa kwenye nyonga, pamoja na kupumzika kitandani mara kwa mara kunaweza kupunguza maumivu ya mgongo.

12.3.2  Maumivu ya viungo

Homoni katika trimesta ya tatu (miezi sita hadi tisa ya ujauzito) huzichochea viungo vya mwanamke na kuzifanya kuwa laini na legevu. Hii hufanya jointi zake ziweze kupindika, zikiwemo jointi kati ya mifupa kwenye pelvisi yake (kumbuka anatomia ya pelvisi katika Kipindi cha 6, hasa Mchoro 6.1).
  • Je, unafikiri ni kwa nini kulegea huku kwa viungo vya pelvisi ni muhimu katika kipindi cha mwisho cha ujauzito?
  • Husaidia kutengeza nafasi inayoweza kupanuka kwenye pelvisi ili mtoto aweze kupita kwenye njia ya uzazi katika leba na kuzaa.
    Mwisho wa jibu
Wakati mwingine, viungo vya mwanamke mjamzito hulegea sana na kuwa zenye kutatiza, hasa nyonga, na huenda akapoteza uthabiti wa pelvisi yake, jambo linalosababisha maumivu. Maumivu ya viungo si hatari, lakini mwanamke anaweza kuteguka kwenye vifundo vya miguu au viungo vingine.

12.3.3  Kukakamaa kwa miguu

Miguu au nyayo za wanawake wengi wajawazito zinaweza kukakamaa – haya ni maumivu makali ya ghafla na kukaza kwa misuli. Kukakamaa huku hasa hutokea usiku au wanawake wanapojinyoosha na kuvuta vidole vyao vya mguu. Ili kukomesha mikakamao, kunja wayo (kuelekea juu) na kisha usugue mguu huo kwa upole ili kuusaidia utulie (usisugue kwa nguvu).
Udhibiti
Ili kuzuia kukakamaa zaidi, mwanamke hafai kukunja vidole vyake kuelekea juu (hata anapojinyosha), na anafaa kula vyakula zaidi vilivyo na kalisi na potasiamu.
  • Je, unaweza kuorodhesha vyakula vilivyo na kalisi?
  • Mboga za manjano kama vile viazi vikuu na karoti, malimau, maziwa, magandi, mtindi, jibini, mboga zenye rangi ya kijani, vyakula vya mifupa na makaka ya mayai, molasi, maharage ya soya na dagaa.
    Mwisho wa jibu

12.3.4  Maumivu ya kighafla katika sehemu ya chini ya upande wa fumbatio

Uterasi, katika nafasi yake, hushikiliwa kwa ligamenti kwa kila upande. Ligamenti ni kiungo mithili ya kamba zinazoshikanisha uterasi kwenye fumbatio la mama. Kusonga kwa ghafla kunaweza kusababisha maumivu makali kwenye ligamenti hizi wakati mwingine. Hii si hatari. Maumivu haya hukoma baada ya dakika chache. Kusugua kwa upole au kuweka kitambaa chenye joto kwenye fumbatio kunaweza kusaidia.

12.3.5  Mikakamao kwenye fumbatio mapema katika ujauzito

Huenda mwanamke huyu ana mimba nje ya uterasi au huenda ujauzito wake ukaharibika. Anafaa kupata usaidizi wa kiafya mara moja.
Ni kawaida kuwa na mikakamao midogo kwenye fumbatio (kama vile mikakamao midogo wakati wa hedhi) wakati mwingine katika trimesta ya kwanza ya ujauzito. Mikakamao hii hutokea kwa sababu uterasi inakua. Hata hivyo mikakamao ya mara kwa mara (inayotokea na kuisha kwa mtindo), au isiyoisha, au yenye nguvu sana na maumivu, au inayosababisha kuvuja damu au matone ya damu ukeni, ni ishara za hatari.

12.3.6  Maumivu ya kichwa na kipandauso

Maumivu ya kichwa hutokea sana katika ujauzito bali si hatari. Maumivu haya ya kichwa yanaweza kuisha mwanamke akipumzika na kutulia zaidi, akinywa juisi au maji zaidi, au akisinga paji la uso kwa upole. Ni SAWA kwa mwanamke mjamzito kunywa tembe mbili za paracetamol na glasi ya maji mara moja baada ya muda fulani. Hata hivyo, maumivu ya kichwa mwishoni mwa ujauzito yanaweza kuwa ishara ya hatari ya priklampsia, hasa ikiwa pia kuna shinikizo la juu la damu, au kuvimba kwa uso au mikono. Priklampsia imejadiliwa kwa kina baadaye katika moduli hii, katika Kipindi cha 19.
Ukishuku kuwa kuna priklampsia, mpe mwanamke rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu mara moja.
Wanawake wengine hupata maumivu ya kipandauso kichwani. Haya huwa maumivu makali ya kichwa, mara nyingi kwenye pande za kichwa. Mwanamke anaweza kuona matone na kuhisi uchefuchefu. Mwanga mkali au mwanga wa jua unaweza kuendeleza maumivu haya. Kipandauso kinaweza kuwa kibaya zaidi katika ujauzito.
Udhibiti
Kwa bahati mbaya, dawa za kipandauso ni hatari sana katika ujauzito. Zinaweza kusababisha leba kuanza kabla ya wakati, na pia zinaweza kumdhuru mtoto. Ni bora kwa mwanamke mjamzito aliye na kipandauso kunywa miligramu 500 hadi 1000 za paracetamol na glasi ya maji kisha apumzike katika chumba chenye giza. Ingawa kahawa na chai si bora katika ujauzito, ni SAWA mara kwa mara, na huenda zikasaidia katika kutibu kipandauso.

12.4 Matatizo madogo katika mifumo mingine ya mwili

12.4.1  Edema

Ukishuku kuwa edema inaweza kuwa ishara ya priklampsia, mpe mwanamke huyo rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu mara moja.
Kuvimba nyayo na vifundo vya miguu hutokea sana katika ujauzito, hasa alasiri au katika hali ya anga yenye joto. Kuvimba huku hutokana na edema,ambayo ni ubakizaji wa viowevu kwenye tishu za mwili. Chini ya nguvu za uzito, kiowevu kilichobakizwa huteremka mwilini na kujikusanya kwenye nyayo. Mhimize mwanamke huyo kuketi akiwa ameinua nyayo zake mara nyingi iwezekanavyo ili kuwezesha viowevu hivi kufyonzeka na kurudi katika mfumo wa mzunguko wa damu. Kuvimba kwa miguu si hatari, lakini uvimbe mkali mwanamke anapoamka asubuhi, au kuvimba kwa mikono na uso wakati wowote, kunaweza kuwa ishara za priklampsia ambayo ni hali mbaya zaidi (hata ya kuhatarisha maisha).
Udhibiti
Mwanamke anaweza kupata nafuu kutokana na uvimbe kwenye miguu akiweka miguu yake juu kwa dakika chache angalau mara mbili au tatu kwa siku, akiepuka kula vyakula tayari vilivyo na chumvi nyingi, na akinywa maji au juisi za matunda kwa wingi.

12.4.2  Ukojoaji wa mara kwa mara

Ukojoaji wa mara kwa mara ni lalamiko la kawaida katika ujauzito, hasa katika miezi ya kwanza na ya mwisho. Hii hutokea kwa sababu fetasi na uterasi inayoendelea kukua hufinya kibofu. Hukoma mtoto anapozaliwa. Ikiwa kukojoa kunasababisha uchungu, mwasho, au kuchomeka, huenda mwanamke huyo ana maambukizi kwenye kibofu. Utambuzi na udhibiti wa maambukizi ya mfumo wa viungo vya mkojo umejadiliwa katika Kipindi cha 18.

12.4.3  Mchozo ukeni

Mchozo ni unyevunyevu utokao ukeni ambao kila mwanamke huwa nao. Mwili wa mwanamke hutumia mchozo huu kujisafisha kutoka ndani. Kwa wanawake wengi, mchozo huu hubadilika wakati wa hedhi. Wanawake wajawazito hupata mchozo mwingi, hasa wanapoelekea mwisho wa ujauzito. Unaweza kuwa angavu au wa manjano. Hii ni kawaida. Hata hivyo, mchozo huu unaweza kuwa ishara ya maambukizi uwapo mweupe, wa kijivu, kijani, wenye viwimbi, wenye harufu mbaya, au uke ukiwasha au ukiwa wenye kuchomeka.
Unafaa kutoa rufaa kwa kila kisa cha maambukizi ya uke kwenda katika kituo cha afya kilicho karibu.

12.4.4  Kuhisi joto au kutokwa na jasho jingi

Kuhisi joto ni jambo linalotokea sana katika ujauzito, na maadamu hakuna ishara zingine za hatari (kama vile ishara za maambukizi), mwanamke huyo asiwe na wasiwasi. Anaweza kuvaa nguo zinazoweza kupitisha baridi, kuoga mara kwa mara, kutumia pepeo la karatasi au jani kubwa, na kunywa maji mengi na viowevu vingine.

12.4.5  Disnia (upungufu wa pumzi)

Wanawake wengi hupata upungufu wa pumzi (hawawezi kupumua kama kawaida) wakiwa wajawazito. Hali hii huitwa disnia.
  • Je, kwa nini unafikiri upungufu wa pumzi ni tatizo linalotokea sana mwishoni mwa ujauzito?
  • Upungufu wa pumzi hutokana na mtoto anayekua kujaza mapafu ya mama na kumkosesha nafasi ya kutosha ya kupumua.
    Mwisho wa jibu
Udhibiti
Wahakikishie wanawake walio na upungufu wa pumzi mwishoni mwa ujauzito kuwa ni jambo la kawaida. Lakini ikiwa mwanamke ni mdhaifu na mwenye uchovu, au akipungukiwa na pumzi kila wakati, anafaa kuchunguzwa kwa ishara za ugonjwa, matatizo ya moyo, anemia, na lishe duni. Pata ushauri wa kiafya ukishuku kuwa huenda ana mojawapo ya matatizo haya.

12.4.6  Ugumu wa kuamka na kulala

Ni vyema mwanamke mjamzito kutolala chali, kwa sababu huenda ikawa vigumu kuamka tena, na kwa kuwa mwanamke akiwa ameulalia mgongo wake, uzito wa uterasi huifinya mishipa mikubwa ya damu ambayo hurudisha damu kwa moyo. Hii inaweza kupunguza usambazaji wa oksijeni kwa ubongo wake kwa muda na kumfanya ahisi kizunguzungu. Ikiwa mwanamke anataka kuulalia mgongo wake, anafaa kuweka kitu chini ya mgongo na chini ya magoti yake ili asilale chali kikamilifu.
Mwanamke mjamzito pia anafaa kuwa makini anavyoamka. Hastahili kuamka kama mwanamke katika Mchoro 12.3 (a). Badala yake, anafaa kugeuka upande mwingine na kujisukuma juu kwa mikono yake, jinsi ilivyo katika Mchoro 12.3 (b).
Mchoro 12.3 (a) Kuamka bila kugeuka upande mmoja kwanza kunaweza kurarua misuli ya fumbatio. (b) Kugeuka upande na kujisukuma juu kwa mikono ni salama sana na atahisi utulivu.

12.4.7  Kloasma (barakoa ya ujauzito)

Tayari unajua jinsi kloasma inavyofanana kutoka katika Kipindi cha 8. Mhakikishie mwanamke kuwa rangi hiyo nyeusi si hatari na kuwa nyingi ya rangi hiyo huisha baada ya kuzaa. Mwanamke anaweza kuzuia kupata madoadoa meusi usoni mwake kwa kuvaa kofia anapotoka nje kwenye jua.

12.5 Hisia na mihemko inayobadilika

Ujauzito ni wakati muhimu katika maisha ya mwanamke. Mtoto anaendelea kukua ndani yake, mwili wake unabadilika, na anahitaji chakula na kupumzika zaidi. Mwili wa mwanamke unapobadilika, uhusiano, ujinsia na maisha yake ya kikazi yanaweza kubadilika pia.

12.5.1  Mabadiliko ya kighafla katika hisia

Ujauzito unaweza kumfanya mwanamke kuwa na mihemko sana. Wanawake wengine hucheka au kulia bila sababu maalum. Wengine huhisi mfadhaiko, hasira, au kuwashwa. Kucheka au kulia kusiko kwa kawaida na mabadiliko mengine ya kighafla ya hisia au mihemko ni kawaida. Haya huisha haraka. Hata hivyo, usipuuze hisia za mwanamke kwa mujibu wa ujauzito wake tu. Hisia zake ni za kweli.

12.5.2  Wasiwasi na hofu

Wanawake wengi huwa na wasiwasi wakiwa wajawazito, hasa kuhusu afya ya mtoto na kuzaa. Wasiwasi wa mwanamke kuhusu matatizo mengine maishani unaweza pia kuongezeka akiwa mjamzito. Wasiwasi kama huu ni kawaida. Haumaanishi kuwa kitu kibaya kitatokea. Wanawake walio na hisia hizi wanahitaji usaidizi wa kihisia, kama vile mtu kusikiza wasiwasi wao na kuwahimiza wahisi wenye tumaini. Pia wanaweza kuhitaji usaidizi wa kutatua matatizo waliyo nayo maishani mwao, kama vile matatizo na wenzi wao, pesa, madawa au pombe, au maswala mengine.

12.5.3  Matatizo ya usingizi

Baadhi ya wanawake wajawazito huhisi usingizi sehemu kubwa ya siku. Hii ni kawaida katika miezi mitatu ya kwanza. Miili yao huwaelekeza kupunguza shughuli na kupumzika. Hakuna haja ya kuingilia isipokuwa mwanamke akihisi udhaifu, ambao unaweza kuwa ishara ya tatizo kubwa zaidi, kama vile ugonjwa, mfadhaiko au anemia.
Wakati mwingine wanawake wajawazito huwa na matatizo ya kulala; wanaweza kuwa na ugumu wa kupata usingizi au waamke baada ya muda mfupi na wasipate usingizi tena. Tatizo hili huitwa insomnia (ukosefu wa usingizi).
Udhibiti wa insomnia
Iwapo mwanamke mjamzito hawezi kulala kwa sababu ya wasiwasi au kuhangaika, anaweza kusaidika:
  • Akilalia upande na kitu cha kustarehesha kati ya magoti yake na kwenye sehemu ya chini ya mgongo wake. Anaweza kutumia mto, blanketi iliyokunjwa, majani ya ndizi, au kitu kingine laini.
  • Mtu akimsinga.
  • Akinywa chai za mitishamba zitakazomsaidia kulala.

12.5.4  Ndoto za ajabu na majinamizi

Huenda wanawake wajawazito wakapata ndoto kubwa dhahiri. Zinaweza kuwa nzuri, za ajabu, au za kutisha. Kwa watu wengi, ndoto ni njia muhimu ya kujielewa na kuelewa dunia. Watu wengine huamini kuwa ndoto zinaweza kueleza kuhusu siku za usoni au kutoa ujumbe kutoka kwa mizimu. Lakini kwa kawaida, kitu kinapotokea kwa ndoto haimaanishi kuwa yatatendeka maishani. Matukio kwenye ndoto yanaweza kuwa yanatueleza yale tunayoogopa, au tunayotamani. Au zinaweza kuwa hadithi tu zinazojitengeneza akilini tukilala. Wanawake wajawazito wanaopata ndoto za kutisha wanaweza kuhitaji mtu wa kuzungumza nao kuhusu matumaini yao, hofu na hisia.

12.5.5  Kusahau

Wanawake wengine wana uwezekano zaidi wa kusahau mengi wakiwa wajawazito. Kwa wanawake wengi, hili si tatizo kubwa. Lakini wengine wanaweza kuwa na wasiwasi ikiwa hawajui kuwa ni kawaida. Hakuna anayejua ni kwa nini wanawake husahau mengi wanapokuwa wajawazito, lakini hutendeka sana.

12.5.6  Hisia kuhusu ngono

Wanawake wengine hawataki kushiriki ngono sana wakiwa wajawazito. Wengine hutaka ngono zaidi. Hisia hizi zote ni za kawaida. Kushiriki au kutoshiriki ngono, yote ni SAWA kwa mwanamke na mtoto wake. Ngono si hatari kwa mtoto. Wakati mwingine ngono si jambo la kuridhisha katika ujauzito. Mwanamke pamoja na mwenzi wake wanaweza kujaribu njia zingine za kushiriki ngono. Inaweza kuwa bora mwanamke akiwa juu, au katika hali ya kuketi au kusimama, au mwanamke akiwa amelalia upande. Mwanamke mjamzito anaposhiriki ngono, ni muhimu kuepusha maambukizi kwa kumshauri kushiriki ngono salama kwa kutumia kondomu ili kuzuia VVU/UKIMWI na maambukizi mengine ya zinaa.

12.6  Hitimisho

Mbinu ulizojifunza awali (katika Kipindi cha 8) zitakuwezesha kuuliza maswali muhimu wanawake wanapokuja kwako kwa huduma ya utunzaji kabla ya kuzaa, ili uweze kugundua ikiwa wana matatizo yoyote madogo unayoweza kuwasaidia kudhibiti. Kuhoji vizuri pia kutadhihirisha ishara za hatari zinazohitaji rufaa kwenye kituo cha afya. Katika kipindi kitakachofuata, utaongeza ujuzi wako wa kuwashughulikia wateja tutakapokufundisha kuhusu masuala katika uendelezaji wa afya utakayohitaji kujadili na wanawake wajawazito katika jamii yako.

Muhtasari wa Kipindi cha 12

Katika Kipindi cha 12, umejifunza kuwa:
  1. Mwili wa mwanamke hubadilika katika ujauzito. Mabadiliko haya wakati mwingine yanaweza kukosesha utulivu, lakini ni ya kawaida na huisha baada ya mtoto kuzaliwa.
  2. Unaweza kupunguza mengi ya matatizo madogo katika ujauzito kwa kupata ushauri kuhusu lishe, mazoezi, na kwa tiba rahisi za nyumbani zinazoaminika kuwa salama na huwasaidia wanawake kuhisi vyema.
  3. Wakati mwingine matatizo haya madogo yanaweza kuwa mabaya, au kuashiria tatizo lingine la kiafya linalohitaji rufaa kwenye kituo cha afya.
  4. Tiba zingine (kama vile dawa za kipandauso) ni hatari kwa wanawake wajawazito na zinaweza kumdhuru mtoto pamoja na mama.
  5. Mtatizo madogo ya ujauzito unayoweza kukumbana nayo unapowahudumia wanawake wajawazito yanaweza kuainishwa kulingana na mifumo ya mwili inayohusika.
  • Matatizo ya utumbo ni kichefuchefu na kutapika, kuchukia baadhi ya vyakula, kiungulio, pika (tamaa ya chakula), uyabisi wa utumbo na hemoroidi.
  • Matatizo ya kiwiliwili cha misuli na ngozi ni maumivu ya mgongo, maumivu kwenye viungo, ugumu wa kuinuka na kujilaza, kuhisi joto au kutokwa na jasho sana, barakoa ya ujauzito (kloasma), maumivu ya kighafla kwenye upande wa sehemu ya chini ya fumbatio, mikakamao mapema katika ujauzito na mikakamao kwenye miguu.
  • Matatizo ya moyo ni uvarikosi na disnia (upungufu wa pumzi).
  • Matatizo ya viungo vya uzazi na vya mfumo wa mkojo ni kukojoa mara kwa mara na mchozo ukeni (unyevunyevu kutoka ukeni).
  • Matatizo ya mfumo wa neva ni kuhisi usingizi na insomnia, maumivu ya kichwa, hisia na mihemko inayobadilika, wasiwasi na hofu, ndoto za ajabu na majinamizi, kusahau, na mabadiliko ya hisia kuhusu ngono.

0 comments:

 

LIKE PAGE YETU UWE WA KWANZA KUPATA HABARI MPYA. Just Click Like Button Below...

Powered By OnlineBlogger