Watumiaji wengi wa huduma ya simu za
mkononi wamekuwa wakilalamikia wizi wa pesa unaofanywa na baadhi ya
makampuni hayo, jana katika kikao cha Bunge Dodoma Serikali imesema
inatambua kuhusu wizi unaofanywa na baadhi ya makampuni ya simu za
mkononi na kutoa tamko namna ambavyo imejipanga kukabiliana na wizi wa
aina hiyo.
Akitoa tamko hilo Naibu Waziri wa
Mawasiliano Sayansi na Teknolojia January Makamba alisema Serikali
itaanzisha kituo maalum cha kushughulikia malalamiko hayo CCC,
kitakachokuwa kinasimamiwa na TCRA.
Akiuliza swali kuhusiana na jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na wizi huo Mbunge wa Konde Khatib Said Haji alisema;
“Wizi huu unaofanywa na
makampuni ya simu si wizi mkubwa kama ule wa ESCROW.. ni wizi mdogo
mdogo unaowaibia Watanzania elfu tano elfu tatu lakini kwa ujumla wake,
Mpemba aliyeko Konde akiibiwa elfu tatu, Mnyamwezi wa Tabora elfu mbili,
Ukizijumlisha ni mamilioni ya shilingi wanaibiwa Watanzania… Leo watu
hao elfu tatu elfu mbili unawaambia wapeleke malalamiko yao, gharama
hiyo umeikadiriaje hata mtu huyo akadai malalamiko ya elfu tatu..”
“Hivi serikali yenu makini
imekuwa wapi muda wote mpaka kukiri kama Watanzania wamekuwa wakiibiwa
na bila wenyewe kujijua?, na bado hamna hatua mlizozichukua, ni nani
aliyeko nyuma ya pazia hili la kuibia Watanzania na ninyi mkaridhia ama
ni yale yaliyosemwa kama CCM ina fund katika wizi huu..?”- Khatib Said Haji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia January Makamba alisema;
“Napenda nikiri tatizo la wizi
au dhuluma kwa wateja lipo na ndio lililopelekea tukaweka hizi kanuni
ambazo zinaweka adhabu na hatua za kuchukua katika kudhibiti wizi huo..
Licha ya utaratibu wa kawaida wa kulalamika katika makampuni ya simu,
kwa sababu moja ya matakwa ya sheria ni kwamba kampuni za simu zinapaswa
kuweka utaratibu wa kuhudumia wateja wake, lakini tumebaini kwamba
utaratibu huo una matatizo, unaweza ukapiga simu muda mrefu isipokelewe,
unaweza kuambiwa usubiri na wakati unasubiri kulalamika pia unakatwa..
“Kwa hiyo Serikali
inafahamu hilo, pamoja na hatua tulizozichukua ni kuweka ule mtambo wa
kufuatilia mawasiliano ambao moja ya kazi yake sio kufuatilia tu mapato
lakini ubora wa mawasiliano.. Kwa kutambua kuwa makampuni ya simu haya
wakati mwingine yanachelewa wakati mwigine yanapuuza wateja, kituo hiki
ambacho tunakianzisha namba zake zitasambazwa kila mtu atakuwa nayo, kwa
hiyo huna haja kusafiri kufuatilia shilingi elfu mbili elfu tatu elfu
tano. Kutakuwa na namba ambayo ni bure kupiga..”- January Makamba.
“ Kila utakapopiga kulalamika
utapewa namba maalum ya lalamiko lako, na lisiposhughulikiwa hata
kitengo cha kampuni ya simu kutoshughulikia lalamiko lako na yenyewe
itakuwa sababu ya makampuni hayo kuadhibiwa..”- January Makamba
Tamko la Serekali Kuhusu Wizi Unaofanywa na Makampuni ya Simu Tanzania Kwa Wateja Wao
Tupe maoni yako hapo Chini..!!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment