Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro
limemtia mbaroni mganga mmoja wa jadi anayedaiwa kuteka watoto kwa njia
za kishirikina kwa ajili ya kutolewa kafara.
Mbali na mganga huyo, pia
wamemtia mbaroni mwanamke mmoja, anayedaiwa kusuka mipango ya kutekwa
nyara kwa watoto na kuwahifadhi kwa mganga huyo.
Mganga huyo ambaye anadaiwa ni
mwenyeji wa mkoani Mbeya, alikutwa na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka
13, akiwa tayari amepumbazwa tayari kumpeleka Mbozi mkoani Mbeya. Mtoto
huyo aliyemaliza darasa la saba mapema mwaka huu Shule ya Msingi
Majengo katika Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa waliofaulu katika
mtihani wa Taifa.
Kwa mujibu wa habari hizo, mganga
huyo (jina tunalo), anadaiwa kushirikiana na mwanamke mmoja, mkazi wa
TPC kula njama za kumteka mtoto huyo. “Huyo mwanamke ndiye alishirikiana
na huyo mganga kumteka mtoto kwa lengo la kumpeleka Mbozi, mkoani Mbeya
na ajabu ni kwamba naye alikuwa akishiriki kumtafuta,” imedokezwa.
Kulingana na chanzo hicho, kiini
cha kugundulika kwa mpango huo ni baada ya mwanamke huyo kwenda na
rafiki yake kwa mganga, ikiwa ni maandalizi ya mwisho kwa ajili ya
kusafiri.
“Walipeleka chakula kwa huyo
mganga na walipoingia ndani ndipo rafiki yake akamuuliza mbona huyu
mtoto, ndiye anayetafutwa,” alidokeza mmoja wa ndugu wa mtoto na
kuongeza:
“Huyo mwanamke ndiyo akamwambia
naomba unyamaze kwa sababu huyu mtoto anasafiri kwenda Mbozi na mganga
na wazazi wake hawatakaa wamwone tena na ndiyo maana nimeleta na hili
begi.”
Hata hivyo, rafiki huyo aliamua
kuvujisha siri hiyo kwa ndugu wa mtoto huyo kuwa amefichwa nyumbani kwa
mganga huyo na ndipo ndugu walipomfuata kwa mganga.
Akizungumza na gazeti hili nje ya
kituo cha kati cha polisi mjini Moshi, Prosper Swai ambaye ni baba
mzazi wa mtoto huyo, alisema mwanaye alitoweka Novemba 2 na baada ya
kutoonekana alitoa taarifa kituo cha Polisi cha TPC na kwa uongozi wa
kijiji na juhudi za kumtafuta hazikuzaa matunda.
Swai alisema baada ya siku tano,
alipata taarifa kwa mtu mmoja kuwa mwanae amehifadhiwa nyumbani kwa
mganga na alipelekwa na mwanamke huyo.
Baada ya kupata taarifa hizo,
akiwa na polisi na uongozi wa kijiji, walivamia nyumba ya mganga huyo na
kumkuta mtoto akiwa amelala chini kwenye mfuko wa mbolea akiwa
hajitambui.
Alifafanua kuwa baada ya kumpata
mtoto huyo, alimkagua na kumkuta na hirizi kubwa kiunoni hali
iliyomfanya aogope kuwa mwanae huyo aliibwa kwa lengo la kutolewa
kafara.
Swai alisema matukio ya wizi wa
watoto katika eneo la TPC na maeneo ya jirani yamekithiri na katika
kipindi cha mwezi mmoja, watoto wanne wamepotea katika mazingira hayo.
Alisema wawili kati yao ni wakazi
wa Kijiji cha Langasani na walikutwa wamekatwa viungo na kutupwa
msituni wakati mtoto mwingine ni wa Kijiji cha Chekereni ambaye bado
hajapatikana.
Mtoto mwingine ni wa Kijiji cha
Mbugani alitoweka juzi baada ya baba yake kumtuma kwenda kukagua tanuru
la matofali na hadi jana mchana alikuwa hajapatikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Geofrey Kamwela alikiri kumshikilia mganga huyo na watu
wengine wanaodaiwa kuhusika kumpeleka mtoto huyo kwa mganga huyo na kuwa
atatoa taarifa baada ya kukusanya taarifa zaidi.
Mtoto Aliyefaulu darasa la Saba Nusura Atolewe Kafara
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment