KIMENUKA! Vigogo wa
madawa ya kulevya wakiwemo viongozi wa dini sasa wanaanza kupukutika
kutoka kwenye mstari wa siri huku baadhi yao wakikimbilia nje ya nchi
kufuatia oparesheni kali inayofanywa na Kikosi cha Kupambana na
Kudhibiti Madawa ya Kulenya Tanzania kuwanasa kila kukicha, Uwazi lina
mchoro kamili.
Hivi karibuni kikosi hicho
kimemkamata askofu (mwangalizi mkuu wa kanisa) aliyetambulika kwa jina
la Emeka Nwachukwu Mert raia wa Nigeria ambaye ana kanisa la kiroho
maeneo ya Sinza jijini Dar.
Jina la kanisa hilo limedhibitiwa na vyombo husika kwa sababu ya uchunguzi zaidi na uhalali wake wa kuwepo nchini.
SIKU YA TUKIO
Vyanzo vyetu makini ndani ya kikosi kazi
vinaeleza kwamba, mchungaji huyo alikamatwa Oktoba 31, mwaka huu saa
kumi usiku Tegeta wilayani Kinondoni, Dar es Salaam akiwa na madawa ya
kulevya ‘unga’ aina ya heroine kilo 35.
KAMA UNGEINGIA SOKONI
Habari za ndani kutoka kwenye oparesheni
hiyo zinasema kuwa, endapo unga huo ungeingia sokoni na kununuliwa,
basi mtumishi huyo wa Mungu angevuna kitita cha zaidi ya shilingi
bilioni mbili.
NYUMBA ALIYONASIWA YA PROFESA
Mchungaji huyo ambaye serikali imeanza
kazi ya kulichunguza kanisa lake, alidakwa na mzigo huo haramu kwenye
makazi aliyopanga ambayo ni nyumba ya profesa mmoja wa chuo kikuu, Mbezi
jijini Dar es Salaam.
WASHIRIKA NAO WADAKWA
Kwa mujibu wa chanzo, kamatakamata ya
mchungaji huyo pia iliwakumba watuhumiwa wengine ambao ni Walyat Khan
raia wa Pakistani, Chuksi Sylvester Agbazuo na Tony Olafor wote raia wa
Nigeria na inadaiwa kwamba walikuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali na
kutoroka.
HABARI NYETI
Habari za siri ambazo Uwazi ilizinasa
zinadai kuwa, watumishi wa Mungu waliokuwa kwenye orodha ya kunaswa
walikuwa wengi lakini wamekimbilia nje ya nchi na kikosi hicho
kimeshawasiliana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kwa ajili ya kuwasaka
na kuwatia nguvuni.
MAJINA MAPYA MEZAN KWA NZOWA
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, Kamanda
wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania,
SACP Godfrey Nzowa amekabidhiwa majina ya vigogo wakiwemo viongozi wa
dini ambao ni sugu katika biashara hiyo. Mbali na majina hayo, pia
amepewa ratiba zao za safari za kibiashara hivyo kilichobaki ni
kuwafuatilia na kuwakamata na ushahidi ili kuhakikisha kwamba hawawezi
kupona mahakamani.
MTANDAO HATARI
Habari zaidi zinadai kuwa, siku za hivi
karibuni, Kamanda Nzowa amekuwa akifumua mtandao wa watu wazito katika
biashara hiyo na imebainika kuwa vigogo hao wana mtandao mkubwa
serikalini ikiwemo wizara ya mambo ya ndani ambao wanawalinda kwa kupewa
mamilioni ya pesa kwa ajili ya usimamizi wa upitishwaji wa biashara
hiyo haramu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
jijini Dar.
“Unajua zamani viongozi hao
serikalini walikuwa wakimsumbua Kamanda Nzowa ili awaachie watuhumiwa
waliokamatwa na unga bila mafanikio, lakini sasa wameshamsoma kiasi
kwamba hata wakikamatwa hawampigii simu tena,” kilisema chanzo kingine.
WATOTO WA VIGOGO
Habari nyingine zinadai kuwa, Kamanda
Nzowa pia ana majina ya watoto wa vigogo wa serikali wanaojihusisha na
biashara hiyo na anayafanyia kazi.
KUMBUKUMBU
Kukamatwa kwa askofu huyo kumekuja baada ya kukamatwa kwa vigogo ambao ni viongozi wa dini katika makanisa ya kilokole.
Januari 11, mwaka huu, Askofu
Moris Charles alidaiwa kukamatwa na polisi maeneo ya Chinga Mbili mkoani
Lindi akiwa na kilo 210 za madawa ya kulevya aina ya heroine yenye
thamani ya shilingi bilioni 9.4, kesi yake bado inaendelea mahakamani
mkoani humo.
Juni 8, 2011 polisi walifanikiwa
kumkamata Mchungaji Kapupu Denis Okechuku wa kanisa la kilokole lililopo
Kinondoni Biafra akiwa na kilo 81 za cocaine, kesi yao bado ipo
Mahakama ya Kisutu, Dar.
KAMANDA NZOWA
Uwazi lilipomtafuta Kamanda Nzowa ofisini
kwake juzi, alisema kuna watu wanne waliokamatwa Tegeta wakiwa na kilo
35 za madawa ya kulevya aina ya heroin na kuna wengine wanatafutwa
kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa sasa nisingependa
kuzungumzia sakata hilo kutokana na sababu za kiupelelezi kwani kuna
wengine tunawatafuta na nitahakikisha wanakamatwa na kufikishwa katika
vyombo vya sheria, nawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao,” alisema
Nzowa.
Aibu! Mchungaji wa Sinza Akamatwa na Madawa ya Kulevya
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment