Matunda na
juisi asilia, vyote vina manufaa, lakini kimoja kinakuwa bora kuliko kingine
kutegemea hali inayomkabili mtumiaji.
Matunda na
mbogamboga ni katika vyakula bora kabisa kutokana na wingi wa vitamin, madini, sukari
ya asilia na virutubisho vingine.
Mtu mwenye
matatizo katika kutafuna anapokunywa juisi ya asilia, anavipata virutubisho
hivyo kwa wingi zaidi katika glasi moja kuliko akila kipande cha tunda ambacho
kitamchosha kutafuna na ashindwe kutumia kwa kiwango kinachotosheleza.
Kwa hiyo
juisi ni chakula kizuri sana kwa mgonjwa ambaye mara nyingi meno yake hayawezi
kutafuna vizuri na mahitaji ya nishati ya mwili wake ni makubwa.
Juisi hasa
iliyotengenezwa na matunda halisi bila ya kuwekwa sukari au yenye sukari kidogo
ni kinywaji kizuri na kina faida kubwa kwa wagonjwa na wenye afya bora.
Juisi
inaongeza maji mwilini, inasafisha damu, inatoa sumu na vitu vingine vibaya
mwilini. Zaidi ya hayo, juisi za matunda
na mbogamboga zinamsaidia mwili kuzalisha mkojo mwingi, hivyo zinasaidia
kuondoa sumu mwilini pale atakapokwenda haja ndogo.
Pia, juisi
ya asilia ni kinywaji mbadala kinachoweza kumuepusha mtu kujenga mazoea ya
kunywa soda au juisi za viwandani.
Kwa upande
mwingine, ulaji wa matunda kwa kutafuna na utumbo kusaga chakula vizuri ni bora
kwake kula matunda badala ya kunywa juisi.
Katika
mchakato wa kutengeneza juisi, baadhi ya virutubisho muhimu vinaharibika,
vinapotea au vinaonekana kuwa ni uchafu na kutupwa.
Baadhi ya
matunda ngozi zake zinaweza kuliwa na ni chanzo muhimu cha virutubisho. Matunda hayo ni kama vile apple, blueberries,
zabibu, strawberries, embe, pera na zambarau.
Ngozi ya
matunda hupokea mwanga wa jua na kutengeneza virutubisho vyenye rangi
mbalimbali ambavyo ni muhimu sana kwa ujenzi na ulinzi wa afya ya binadamu.
Mfano wa
virutubisho hivyo ni carotenoids na flavonoids ambavyo vinasaidia kuimarisha
kinga na afya ya mwili kwa ujumla.
Vitamin C inahitaji uwepo wa flavonoids ili kufanya kazi vizuri mwilini.
Ngozi ya
matunda kama zabibu zinasaidia kulinda afya ya ngozi ya binadamu na kupunguza
hatari ya mtu kupata ugonjwa wa saratani.
Ngozi na
nyama za ndani za matunda kama machungwa ni chanzo kizuri cha nyuzi lishe,
ambazo hupotea wakati wa kuchuja juisi.
Nyuzi lishe
zinasaidia usagaji wa chakula tumboni, humwezesha mtu kupata haja kubwa na
kuepuka saratani ya utumbo mpana.
Zinapunguza pia kasi ya sukari kutoka katika utumbo na kuingia katika
damu, na zinapunguza wingi wa nishati.
Kwa hiyo
nyuzi lishe zinachangia kupunguza hatari ya mtu kupata ugonjwa wa kisukari,
unene na uzito kupita kiasi.
Ulaji wa
matunda na mbogamboga unajaza tumbo na kumfanya mtu kujisikia ameshiba kwa muda
mrefu. Juisi inaleta shibe ya muda mfupi
na kuongeza nishati mwilini kwa haraka.
Ili kupata
manufaa ya matunda na juisi asilia, watu wale matunda na mboga za majani aina
tofauti kila siku. Pia, wanywe juisi
asilia glasi moja kwa siku au kila baada ya siku mbili.
Tahadhari ni
kwamba; imethibitishwa kisayansi kuwa unywaji wa juisi uliokithikiri unaweza
kuchochea ugonjwa wa kisukari kwa wakubwa na watoto, unene na uzito kupita
kiasi.
0 comments:
Post a Comment