MTU ambaye
ametajwa kuwa ni gaidi mwenye asili ya Kisomali (jina lake
halikupatikana) ambaye imeelezwa alijeruhiwa kwa risasi katika mapambano
kati ya magaidi na
askari wa Kituo cha Polisi Stakishari, Dar Julai 12, mwaka huu, amefariki dunia na kuzikwa kwa siri, Uwazi liko kazini.
Baada ya
kifo hicho, inadaiwa magaidi wenzake waliuzika mwili wake kwenye kaburi
hilo lililopo kwenye msitu wa Kijiji cha Mamndikongo, Mkuranga, Pwani
bila wanakijiji kujua.
UWAZI LIMECHIMBA HIVI
Taarifa
zilizopatikana toka vyanzo vyetu makini katika kijiji hicho zinadai
kwamba, kaburi la gaidi huyo liligundulika Jumatatu iliyopita. Na hatua
chache mbele zikapatikana bunduki mbili aina ya SMG sanjari na risasi
kadhaa kufuatia msako mkali ulioendeshwa na wanakijiji kwa ushirikiano
wa polisi.
Askari na
wananchi eneo la tuikoMara baada ya taarifa hizo, Uwazi lilifunga safari
hadi kijijini hapo kwa lengo la kuujua ukweli ambapo Mtendaji wa Kijiji
cha Mamndikongo, Issa Said Mchalaganga alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli
kuna msako mkali unaoendeshwa na askari polisi, vyombo vya usalama kwa
ujumla na wananchi wa kijiji hiki ambapo Jumatatu iliyopita tulifukua
sehemu tuliyoitilia shaka na kukuta mwili wa mtu mwenye asili ya
Kisomali.”
HALI YA MAITI
“Maiti
tuliikuta imevaa t-shirt yenye alama ya pundamilia, jaketi lenye
maandishi ya King Lion (mfalme simba), bukta, pensi, trak’suti ya
kuteleza na raba na ilionesha ni mtu mwenye asili ya Somalia kutokana na
nywele na sura. Pia alikuwa na madevu.
“Alikuwa
pande la mtu, mwenye kifua kipana. Tulipomwangalia vizuri alionekana
kuwa na urefu wa kama futi 5.8 na umri tulioukadiria kuwa ni kati ya
miaka 45 hadi 50.”
KISA CHA MSAKO
“Tulianza
msako mkali katika maeneo ya mashamba ya watuhumiwa hao ambao baadhi yao
wamekamatwa na wengine kukimbia nyumba zao baada ya kugundua kuwa,
wanasakwa na polisi. Hii ni kufuatia kurejea kwao kijijini hapa nyakati
za usiku wa saa tatu kwa siku tatu kabla ya maiti hii kupatikana.
“Taarifa
tulizozipata ni kuwa, siku hiyo walifika usiku na pikipiki zaidi ya sita
na kuziegesha sehemu iliyokuwa makazi yao kwa lengo la kwenda kwenye
maskani yao ya zamani. Lakini walipofika karibu na nyumba ya mtu
anayeitwa Joseph Chacha, mbwa wa hapo alibweka wale magaidi wakampiga
risasi na kufa. Waliposonga mbele walimuona mbuzi akipita, wakafikiri ni
mbwa, naye wakampiga risasi, akafa.”
WAKUTA MAZINGIRA TATA
“Taarifa
tulizozipata ni kwamba waliposonga mbele walikuta mazingira ya sehemu
waliyokuwa wakiishi yamebadilika. Kulifyekwa hali ilyowafanya wapatwe na
hofu na kuamua kuondoka.
“Baada ya
taarifa hizo, ndipo sisi tuliwasiliana na polisi na kwenda kuangalia
kilichowaleta. Sasa katika msako wa kutafuta tukaona hilo kaburi.”
BENDEJI YAZUA MASWALI
Mtendaji
huyo alizidi kusimulia: “Pia tulifukua dawa na bendeji ambayo ilikuwa na
masalia ya damu hali iliyoashiria kwamba, alikuwa akitibiwa majeraha ya
risasi akashindwa kupata nafuu kwani. Sehemu za mwili wake hasa zile
zilizoingia risasi ziliharibika sana.
Silaha zilizokutwa karibu na kaburi la gaidi huyoMAGAIDI WANA DAKTARI WAO
“Daktari
alikuja akaufanyia uchunguzi mwili kisha akaruhusu uzikwe tena. Lakini
pia kwa upande wao, inasemekana watu hao pia wana daktari wao ambaye
alikuwa akiwatibu pale wanapojeruhiwa wakati wa mapambano, sasa na yeye
ametoweka.”
KWA NINI MAGAIDI BADO WANARUDI KIJIJINI?
“Watu hao
wanaonekena kutafuta namna ya kurudi hapa kijijini kwa sababu kuna vitu
vyao, zikiwemo silaha walizoficha ardhini sehemu mbalimbali ila
wanashindwa kuja moja kwa moja.”
WANAKIJIJI WASHINDA KWA HOFU
Naye
Mkufunzi wa Mgambo Kata ya Bupu na Kamanda wa Kijiji cha Mamndikongo, MG
357062 Abdallah Twalib Mandale alisema kwa sasa wananchi wa kijiji
hicho wana hofu kiasi kwamba wanashindwa kuendelea na shughuli zao ili
kushiriki katika msako wa silaha za magaidi hao.
WANAKIKIJI WAPONGEZA
Hata
hivyo, wanakijiji hao walimpongeza Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova na vyombo vyote vya ulinzi na usalama
ambavyo vimekuwa vikiendesha oparesheni hiyo ambayo imeleta mafanikio
makubwa pia wameiomba serikali kuwapatia vyakula na maji askari
wanaojihusisha na zoezi hilo kwani wamekuwa wakifanya kazi porini kwa
muda mrefu bila kula wala kunywa maji jambo ambalo ni hatari.
0 comments:
Post a Comment