Mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja, Yadiko Chigoda amelazwa
katika Hospital ya Benjamini Mkapa Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma baada
ya kupigwa na mchi kichwani na baba yake mzazi na kumsababishia maumivu
makali.
Akizungumza mama mzazi wa mtoto huyo, Carolina Mnyawami ambaye ni
mkazi wa kijiji cha Mingui kata ya Lumuma Wilayani Mpwapwa amesema tukio
hilo limetokea leo majira ya saa 4 asubuhi ambapo mume wake
aliyefahamika kwa jina la Fabian Chigoda alikuwa anapigana na kaka yake
hivyo aliamua kuwaamulia ugomvi wao.
Amesema katika ugomvi huo walikuwa wanapigana na fimbo, hivyo
alipowanyang’anya fimbo hiyo ili wasiendelee kupigana ndipo (Chigoda)
alipoamua kuchukua mchi ili ampige nao mkewe kichwani lakini alikwepa na
alipourusha ndipo ulipompata mtoto huyo kichwani.
“Nilipowanyang’anya fimbo ili wasiendelee kupigana, mume wangu aliokota
mchi na kunirushia kichwani.. kwa bahati nzuri niliuona mchi huo na
kukwepa ili usinipige ndipo ulipompiga kichwani mwanangu niliyekuwa
nimembeba mgongoni,” amesema Carolina.
Ameongeza kuwa, “Baada ya kuona kuwa amempiga mtoto alikimbia na hajulikani alipo mpaka sasa.”
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Said Mawji amethibitisha kumpokea
mtoto huyo na kwamba hivi sasa mtoto huyo anaendelea kupata tiba na
uchunguzi zaidi wa afya yake.
“Ameumia sana kichwani lakini bado tunampatia tiba na uchunguzi zaidi
kwenye fuvu la kichwa, kwani inaonekana kama vile limepasuka,” amesema
Dk, Mawaji.
Hata hivyo amesema kuwa wanafanya mpango wa kumpa rufaa mtoto huyo ili
aweze kwenda kutibiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mingui, Mwingwa Udoba amesema chanzo cha
tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia na kwamba bado wanamtafuta baba mzazi
wa mtoto huyo kwa kuwa alikimbia baada ya tukio hilo.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alipotafutwa
kuzungumzia tukio hilo simu yake ilipokelewa na mtu aliyesema kuwa
Kamanda alikuwa kwenye kikao cha kazi.
Maskini :Mtoto Mchanga Apigwa na Mchi Kichwani Dodoma
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment