Vunja jungu! Saa kadhaa kabla ya kuanza kwa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani, jamaa aliyetajwa kwa jina moja la Lugali ameibua
sekeseke kwenye nyumba ya kulala wageni (gesti), kisa kikidaiwa ni
mchepuko akihusishwa na mke wa mpangaji wake, Ijumaa Wikienda lina kisa
na mkasa.
Wakati ikirandaranda mitaani kutega mingo, Timu ya Oparesheni Fichua
Maovu (OFM) ya Global Publishers ilipokea mchongo kuwa kuna timbwili
kwenye gesti moja maeneo ya Buguruni, Dar ambapo walifika eneo la tukio
na kushuhudia kasheshe hilo la aina yake.
OFM ilimshuhudia mzee huyo akichomolewa kutoka chumbani huku damu
zikimvuja baada ya kula kichapo kutoka kwa jamaa na ndugu wa mwanaume
aliyedai kuwa jamaa huyo alikuwa anamsumbua mkewe.
Walidai kwamba mzee huyo ambaye ni baba mwenye nyumba, alikuwa akimtolea udenda mke huyo wa mpagaji wake ambaye ni jirani yake huku akimsumbua mara kwa mara kwa simu na ujumbe mfupi wa SMS.
Ilidaiwa kwamba kufuatia usumbufu huo, mke huyo alimweleza mumewe lakini mumewe hakuamini kama kweli baba mwenye nyumba alikuwa akimtaka mke wake kimapenzi.
Ilisemekana kuwa mume huyo alimweleza mkewe ili aamini kweli baba mwenye nyumba alipania kumtaka basi amkubali ili amkute naye gesti amkomeshe kwa tabia hiyo ya baadhi ya wenye nyumba ambao huwataka wake wa wapangaji wake.
“Nilimwambia mke wangu amkubali kwa sababu nilikuwa na nia ya kukomesha tabia yake ya kutongoza wake wa wapangaji wake, akamwita Buguruni ndipo nikawapigia ninyi waandishi wa habari ili mje mchukue ushahidi,” alisema mume huyo.
Baada ya kukutwa gesti humo, mzee huyo aliomba msamaha kwa mpangaji wake huyo na kuahidi kulipa fidia ambapo aliwaandikia cheki feki kisha akakimbilia Kituo cha Polisi cha Buguruni na kufungua shauri kuwa alitekwa, akapigwa kisha akapelekwa gesti.
Shauri hilo ambalo liliandikishwa kwa jalada namba BUG/RB 6182/2014- utekaji. Mzee huyo alidai kutekwa na mpangaji wake huyo na kumpeleka nje ya mji kisha kumpiga ili kuua soo.
Hadi gazeti hili linaanua jamvi kituoni hapo, polisi walikuwa wakichunguza ili ukweli ujulikane.
0 comments:
Post a Comment