Migogoro katika mahusiano ya mapenzi ni kitu cha kawaida kutokea. Wenza katika mahusiano hugombana na ugomvi mwingine hupelekea hadi kupigana na kusababishiana maumivu hata kuumizana.
Lakini migogoro mingi inaweza kuepukika kama tu wenza hao wakitambua vitu vinavyosababisha kugombana kwao na kuweka mikakati itakayowasaidia kuishi kwa amani zaidi na kuifuata.
Mara nyingi katika mahusiano ugomvi hausababishwi na ujumbe au mawazo tofauti yanayotolewa na mmoja wao bali namna ujumbe huo unavyotolewa na jinsi mpokeaji anavyotafsiri.
Hii inamaana kuwa kama wenza hao wakikubaliana na wakawasiliana hoja zao katika namna ambavyo kila mmoja wao anahisi kusikilizwa na kujaliwa namba za magomvi zitapungua sana.
Hebu tuone namna ambavyo migogoro katika mahusiano inaweza kupunguzwa na kusuluhishwa:
Mbinu # 1: Acha Kujihami
Mapambano kati ya wenza wawili yanaweza kufananishwa na mpambano wa mchezo wa ngumi. Bondia mmoja anapotupa makonde mfululizo na mwingine anajaribu kuzuia ni kawaida atakuwa narudi nyuma na kuruhusu mwenzake aendelee kumvamia.
Vivyo hivyo katika ugomvi katika mahusiano ya wapenzi. Mwenza mmoja napomvamia mwenzake kwa maneno makali na tuhuma kwa mfano, na mwingine akawa anajihami nayo kwa kupinga au kwa kurudisha tuhuma,kinachotokea ni kuwa mapambano yataendelea.
Kama unatengeneza mazingira ya kujihami na mpenzi wako basi unafanya aendelee kukushambulia na hivyo kuendeleza mgogoro kwa muda mrefu.
Zuia kujihami na toka katika uringo wa mapambano. Kumbuka bondia hawezi kupigana na upepo,kama hakuna mpinzani basi hakuna pambano.
Epuka majibizano ya maneno ambayo yatapelekea ugomvi. Kuwa wa kwanza kukaa kimya,ikiwezekana kuondoka kwa muda huo na muendelee mazungumzo baadae wakati kuna utulivu na kusikilizana.
Mbinu # 2: Toa Nafasi ya Kusikiliza
Kuna haja kubwa kwa binadamu yeyote kupenda kusikilizwa na kueleweka.
Mpenzi wako anapokuwa amekasirika au amepandwa na jazba au ameumizwa kihisia anapenda kusikilizwa shida yake na apate kueleweka.
Unahitaji kutoa nafasi ya kusikiliza na kuelewa nini anafikiri au kuhisi moyoni. Jaribu kurudia kile alichosema kumhakikishia kuwa umemsikia vizuri. Pia inaonyesha kuwa unajali. Mpenzi yeyote anapenda kuona kuwa mawazo yake na yeye mwenyewe yanajaliwa.
Unaporudia kutamka alichosema kuna maana mbili, ya kwanza ni kuwa umemsikia vizuri lakini pili ni kuwa inaonyesha kuwa unajali.
Mfano: “Najua jambo hili ni muhimu kwako,lakini nafikiri tungeangalia mambo yanayohusu watoto na mahitaji yao kwanza na hilo lifanyike baade”
Jaribu mbinu hii kwa mwenza wako mnapokuwa na migogoro na uone jinsi inavyofanya maajabu.
Kumbuka sauti inayotumika iwe yenye kuonyesha kujali na sio kuongea kama vile ni polisi.
Mbinu # 3: Chukua Wajibu
Tatizo linapotokea na likazusha mgogoro ni jambo la busara kwa mmoja wenu kukubali kuwajibika katika suala hilo na sio kurushiana lawama kila mmoja akimlaumu mwenzake kuwa amekosea.
Kama mmoja wao akikubali kuwa ni kosa lake,hakutakuwa na ugomvi tena. Wengine hukubali kosa hata kama si lao ilimradi tu kuwe na amani. Utasikia mtu akisema “Nakubali yaishe..”
Mfano:
i. Mapambano
Mke: “Tumelala bila kufunga milango leo,kwanini hukuangalia milango kabla hatujalala?”Mme: ”Hilo ni tatizo lako,kwanini wewe ndio ulikuwa wa mwisho kuingia”
ii. Kuwajibika
Mke: “Tumelala bila kufunga milango leo,kwanini hukuangalia milango kabla hatujalala?”Mme: ”Ahh.. Samahani! Ni kweli kama baba wa nyumba ni jukumu langu kuhakikisha usalama wa nyumba. Nitakuwa makini zaidi,ni kosa langu”
Katika mfano wa kwanza ni lazima mabishano yataendelea,na usishangae yakaishia hata kupigana. Lakini katika mfano wa pili,mgogoro umeisha,sana sana watacheka na kukumbatiana.
Mbinu # 4: Kusimama Pamoja
Mapambano mengi baina ya wapenzi husababishwa na kuvunjika kwa mawasiliano. Kunasababishwa na kutoelewa madhumuni ya mwenza wake.
Kutoelewana ni adui ambaye anaweza kuwasambaratisha wapenzi,na wakaharibu mahusiano yao.
Ni muhimu sasa kwa wapenzi kwa pamoja kushambulia KUTOELEWANA.
Kutoelewana kunapotokea ni muhimu kupeana nafasi ya kufafanua maana ya maneno yake ya awali au matendo yake.
kwa namna hii utaweza kufahamu madhumuni yake.
Kufaninisha hili ni lazima kuwa msikivu(Mbinu #2) vinginevyo utakosa kusikia ufafanuzi wake.
Ni muhimu kutumia neno “SISI” na siyo “MIMI” katika kufafanua mazungumzo yenu.
Mfano:
Mme:”Ni kweli tumelala bila kufunga milango,ila wote tulikuwa tumechoka sana na kazi za siku nzima,tuwe waangalifu zaidi siku zijazo”
Fanyia Kazi..:
Hebu tumia mbinu hizi nne rahisi kabisa katika kutatua migogoro katika mahusiano yako, ni hakika kuwa utafanikiwa sana na kuleta amani na maelewano na mweza wako.Kumbuka hakuna mshindi katika mabishano yanayotokea katika mahusiano yako,wote mnapoteza. Mkilitamba hili kwapamoja mtasimama pamoja na mtaangalia mbinu sahihi ambazo zimetajwa katika makala hii kuwasaidia kuondokana na migogoro katika mahusiaono yenu.
Je huwa unagombana na mpenzi wako mara kwa mara? Najua jibu la wengi ni ndiyo. Basi jaribu mbinu hizi nne zilitotajwa na uone matokeo yake.
Kama una maoni juu ya mada hii,tuandikie mawazo yako katika kisanduku cha maoni hapa chini . Pia tutumie mbinu nyingine ambazo unazitumia na zinafanya kazi ili tufaidik
0 comments:
Post a Comment