OLIVER OSWALD NA ESTER MNYIKA, DAR ES SALAAM,
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), imeziondoa sokoni na kuzifutia usajili aina tano za dawa zinazotumiwa na binadamu baada ya kugundulika kuwa zina madhara katika mwili wa binadamu.
Sambamba na hatua hiyo, pia imepiga marufuku uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa hizo.
Uamuzi huo ulitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam.
Sillo alisema mamlaka yake ilifanya uchunguzi kwa kufuatilia kupitia mifumo yake ya usalama na ubora wa dawa na kubaini kuwa dawa ya vidonge vya kutibu maradhi ya fangasi inayojulikana kwa jina la kapsuli aina ya Ketoconazole, dawa ya maji na vidonge ya kutibu malaria aina ya Amodiaquine au Amodium (Monotherapy) na dawa za maji na vidonge za kutibu mafua na kikohozi, aina ya Kapsuli zenye viambato hai aina ya Phenylpropanol amine zina madhara na hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Nyingine ni dawa za sindano za kuua bakteria aina ya Chloramphenicol Sodium Succinate inayotengenezwa na Kiwanda cha Lincoln Pharmaceutical Ltd cha nchini India, pamoja na dawa ya maji na kapsuli ya kuua bakteria aina ya Cloxacillin ambazo pamoja na zilizotajwa hapo juu zimekuwa zikipoteza ubora wake haraka kabla ya muda wake kumalizika (expire date).
Sambamba na hayo, TFDA pia imebadilisha matumizi ya dawa nne, ikiwemo dawa ya vidonge yenye mchanganyiko wa Sulphadoxine na Pyrimethamine inayofahamika zaidi kama SP, iliyokuwa ikitumika kutibu ugonjwa wa malaria, ambayo kwa sasa itatumika kama kinga ya ugonjwa huo kwa wajawazito pekee.
Aidha, TFDA imebadilisha matumizi ya dawa aina ya Kanamycin, Amikacin na Levofloxacin, zilizokuwa zikitumika kutibu ugonjwa wa kifua kikuu katika hospitali, zahanati na vituo vya afya pekee ili kukomesha utumiaji holela wa dawa hizo ambazo zikizoeleka mwilini husababisha usugu wa ugonjwa.
“Tumewaagiza watoa huduma za afya nchini kuacha kutoa dawa zilizofutiwa usajili kwa wagonjwa na kuzirudisha kwa wasambazaji. Pia watoa huduma wanapaswa kusimamia mabadiliko ya matumizi ya dawa aina ya SP ili zitumike kwa wajawazito pekee na dawa aina ya Kanamycin, Amikacin na Levolfoxacin wazitoe kwa wagonjwa wa kifua kikuu tu ndani ya hospitali, zahanati au vituo vya afya na siyo maduka ya dawa.
“Tumewataka waendelee kutoa dawa aina ya Cloxacillin pekee hadi hapo itakapomalizika kwenye soko kwa sababu matoleo yaliyopo yalishapimwa na kuthibitishwa kukidhi vigezo na ubora,” alisema Sillo.
Alisema kuondolewa kwa dawa hizo katika soko hakutaathiri tiba kwa vile zipo dawa mbadala zinazoweza kutibu magonjwa yanayotibiwa na dawa za aina hiyo.
Wakati huo huo, Sillo aliwataka watengenezaji wa dawa na wasambazaji kuhakikisha wanatengeneza dawa zinazokidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi kwa mujibu wa sheria ya chakula, dawa na vipodozi, sura ya 219.
“Watakaobainika kuingiza na kusambaza dawa zilizofutiwa usajili watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa sababu agizo hili limezingatia mabadiliko ya mwongozo wa sera ya upimaji ya mwaka 2013 iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,” alisema Sillo. mtanzania fikra yakinifu
0 comments:
Post a Comment