zikiwemo supu ya mifupa (bone marrow) na mfumo wa lymph (lyphatic system). Kwa maneno rahisi, leukemia humaanisha saratani ya damu. Kuna aina mbalimbali za leukemia, nyingine zikiathiri watoto na nyingine zikiathiri zaidi watu wazima.
Kwa kawaida leukemia huanzia kwenye chembe nyeupe za damu yaaniwhite blood cells, ambapo mwili huzalisha kiwango kikubwa cha seli zenye maumbo mabaya ambazo hazina uwezo wa kufanya kazi zake sawasawa. Kazi ya chembe nyeupe za damu ni kulinda mwili dhidi ya vimelea waletao maradhi mbalimbali.
Leukemia husababishwa na nini? Kama zilizo kwa aina nyingi za saratani, mpaka sasa chanzo halisi cha leukemia hakijulikani. Hata hivyo, wanasayansi wanadai kuwa leukemia hutokea kutokana na mkusanyiko wa vyanzo mbalimbali vikiwemo vinavyohusu sababu za kinasaba (genetic factors) na kimazingira.
Kwa ujumla, leukemia hutokea pindi chembe nyeupe za damu zinapobadilika muundo wake wa kinasaba yaani viasili vyake vya DNA, ambavyo kwa kawaida hubeba maelekezo yanayoifanya seli yeyote ya kiumbe hai iweze kuishi, kutenda kazi zake, kujizaa na hata kufa, vinapobadilika maumbile na muundo wake kutokana na sababu mbalimbali. Kitendo cha kubadilika kwa maumbile na muundo wa DNA hujulikana kama mutation. Ndiyo kusema basi, seli yeyote iliyopatwa na tatizo hili huwa na tabia ya kukua kwa haraka na kujizaa (kujigawa) kwa kasi zaidi kuliko kawaida, na pindi inapofikia muda wake wa kufa seli hiyo hugoma kufa badala yake huendelea kujizaa zaidi hatimaye kusambaa kwa wingi katika mfumo mzima wa damu, hali inayosababisha saratani ya damu.
Je, kuna vihatarishi vya leukemia?Ndiyo vipo! Pamoja na kwamba chanzo halisi cha saratani ya damu hakijulikani, lakini kuna mambo ambayo humuongezea mtu hatari ya kupata ugonjwa wa saratani ya damu.
Mambo ambayo yanaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya damu ni pamoja na:
Historia ya matibabu ya saratani hapo kabla: Watu ambao wamekuwa kuwa na aina nyingine za saratani hapo awali, na wakati wa matibabu wakapewa tiba ya mionzi au madawa makali ya saratani, wapo katika hatari kubwa ya kupata saratani ya damu kwa sababu baadhi ya dawa hizi pamoja na mionzi huwa na tabia ya kuathiri pia seli nyeupe za damu pamoja na tishu zinazotengeneza seli hizo.
Kuwa na magonjwa mengine ya vinasaba:
Ingawa haieleweki sawasawa uhusiano wake ulivyo, kuwa na baadhi ya magonjwa ya kinasaba kama vile ugonjwa wa Down syndrome, yasemekana huongeza uwezekano wa muathirika kuugua pia ugonjwa wa saratani ya damu.
Baadhi ya magonjwa mengine ya damu:
Watu wenye magonjwa mengine ya damu kama vile ugonjwa wa damu unaoshambulia tishu za supu ya mifupa na kuzifanya zizalishe seli nyingi za damu bila uwiano unaotakiwa yaanimyelodysplastic syndromes, huongeza pia uwezekano wa mtu kuugua saratani ya damu.
Kupigwa na kiasi kikubwa cha mionzi:
Watu ambao wamewahi kupigwa na kiasi kikubwa cha mionzi kama vile mlipuko wa mabomu au kulipuka kwa vinu na mitambo ya nuklea (nuclear reactors), wana hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya damu pamoja na saratani nyingine.
Kupigwa/kutumia baadhi ya kemikali:
Watu waliowahi kukumbana na baadhi ya kemikali kama vile benzene au zile zinazotumika kwenye viwanda vya kuyeyusha vyuma au kutengeneza magurudumu au mabomba ya plastic, nao pia wapo katika uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya damu.
Uvutaji sigara: Jambo hili pia huongeza uwezekano wa kupata aina mojawapo ya saratani ya damu.
Kuwa na historia ya ugonjwa huu katika familia:
Watu ambao, baadhi ya ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu, nao pia wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya damu. Hata hivyo, hii haina maana kwamba leukemia inaambukizwa isipokuwa kuna uhusiano wa kifamilia tu katika kusababisha ugonjwa huu.
Jambo moja la kufahamu ni kuwa, wapo watu wengi ambao wamewahi kukumbana na vihatarishi nilivyovieleza hapo juu bila kupata leukemia, kadhalika wapo waliopata leukemia bila kukumbana na kihatarishi hata kimoja kati ya hivi. Kwahiyo. Uwepo wa vihatarishi hivi haimaanishi kuwa ni lazima mtu apate leukemia isipokuwa inaongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu.
Makundi ya leukemiaWataalamu
wa afya wanaiainisha leukemia katika makundi mbalimbali kulingana na
kasi ya kusambaa kwa ugonjwa pamoja na aina ya chembe damu
zilizoathirika.
Kulingana na aina ya chembe damu zilizoathirika, leukemia inaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili, ambayo ni:
Leukemia inayoathiri zaidi chembe damu zinazounda mfumo wa lymph ambayo kwa kitaalamu huitwa Lymphocytic leukemia. Mfumo wa lymph au lymphatic system ndiyo unaolinda mwili wako dhidi ya maradhi na maambukizi mbalimbali kama vile VVU n.k. Chembe damu zinazohusika hapa huitwa lymphocytes.
Leukemia inayoathiri zaidi chembe/seli zinazounda chembe damu nyingine za mwili yaani kwa kitaalamu Myelogenous leukemia. Aina hii ya leukemia huathiri chembe zinazoitwamyeloid cells, ambazo ndizo huzaa chembe nyekundu za damu, chembe nyeupe za damu pamoja na chembe sahani. Chembe nyekundu husaidia kusafirisha hewa safi ya oksijeni mwilini na kutoa hewa chafu ya kabondioksaidi, chembe nyeupe hupambana na vimelea wa magonjwa mbalimbali kama vile uti wa mgongo, minyoo, kifua kikuu, nk., wakati chembe sahani husaidia kuganda kwa damu pindi mtu unapoumia au kujikata.
Njia ya pili ya kuainisha makundi ya leukemia ni kwa kuangalia kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa saratani ya damu mwilini mwa muathirika. Kwa njia hii, kuna makundi makuu mawili ya leukemia, ambayo ni:
Leukemia inayosambaa kwa haraka au wataalamu wanaitaacute leukemia. Katika aina hii, chembe damu huwa changa, zenye mambo mabaya yasiyo ya kawaida, na zisizoweza kufanya kazi zao vizuri. Lakini mbaya zaidi, hujigawa na kuzaliana kwa kasi kubwa kiasi cha kusambaa na kujazana katika damu kwa muda mfupi sana.
Leukemia inayosambaa taratibu au kwa kitabibu chronic leukemia. Katika aina hii, chembe damu huwa zimekomaa na zenye uwezo wa kujigawa na kuzaliana taratibu na hata kufanya kazi zake kama kawaida. Chembe damu huweza kuishi kwa muda mrefu bila hata mgonjwa kuonesha dalili yeyote ya kuugua leukemia.
Aina za Leukemia
Bila kujalisha kasi ya kusambaa kwa ugonjwa au aina ya chembe damu iliyoathirika, leukemia inaweza kugawanywa katika aina zifuatazo:
Leukemia inayosambaa kwa haraka huku ikishambulia chembe damu zinazounda mfumo wa lymph yaani Acute lymphocytic leukemia (ALL). Aina hii huwapata zaidi watoto wenye umri mkubwa kidogo ingawa pia inaweza kwa kiasi fulani kuwapata hata watu wazima.
Leukemia inayosambaa kwa haraka huku ikishambulia chembe/seli zinazounda chembe damu nyingine za mwili yaaniAcute myelogenous leukemia (AML). Aina hii ya leukemia inaongoza kati aina nyingine zote na huwapata watoto pamoja na watu wazima.
Leukemia inayosambaa taratibu huku ikishambulia chembe damu zinazounda mfumo wa lymph yaani chronic lymphocytic leukemia (CLL). Aina hii huwapata zaidi watu wazima, na nadra sana kutokea kwa watoto. Wagonjwa wa aina hii ya leukemia huweza kuishi vizuri kabisa bila kuwa na dalili zozote zile.
Leukemia inayosambaa taratibu huku ikishambulia chembe/seli zinazounda chembe damu nyingine za mwili yaanichronic myelogenous leukemia (CML). Watu wazima ndiyo waathirika wakubwa zaidi wa aina hii ya saratani ya damu. Mtu mwenye aina hii ya leukemia anaweza akapata dalili chache au asiwe na dalili kabisa kwa miezi hata miaka kabla ya ugonjwa kufumuka ghafla na kuanza kumshambulia.
Dalili za leukemia ni zipi?
Dalili za leukemia hutofautiana kutoka aina moja mpaka nyingine. Hata hivyo, dalili za jumla za leukemia ni pamoja na;
Homa au kujihisi baridi
Uchovu na ulegevu wa mwili
Maambukizi ya mara kwa mara
Kupoteza uzito bila kukusudia
Kuvimba tezi za mitoki
Kuvimba wengu (splenomegaly)
Kuvimba ini (hepatomegaly)
Kutokwa damu kirahisi na kupata michubuko ya mara kwa mara
Kuvilia kwa damu chini ya ngozi
Kutokwa jasho kupita kiasi hasa nyakati za usiku
Kuhisi maumivu ya mifupa
Kupungukiwa damu mara kwa mara
0 comments:
Post a Comment