SERIKALI YAVUNA AIBU KWA DK ULIMBOKA...

Dk. Steven Ulimboka.
 
  Aliyeshtakiwa juu yake hahusiki kabisa
  Mahakama ya Kisutu yamfutia mashtaka
  Polisi wamng'ang'ania kwa kuwadanganya.
Ni kama Serikali imevuliwa nguo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumwachia huru raia wa Kenya, Joshua Gitu Mhindi (32), aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutaka kumsababishia kifo, Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.

Hata hivyo, baada ya kuachiwa huru, alikamatwa tena na kusomewa shtaka jipya la kutoa taarifa za uongo katika kituo cha Polisi Oysterbay, kwamba alimteka nyara Dk. Ulimboka.

Mshtakiwa huyo alidaiwa kufanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 122, cha kanuni ya adhabu.

Raia huyo wa Kenya, aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumteka na kujaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka, aliachiwa huru mbele ya Hakimu Warialwande Lema na kufunguliwa shauri jipya mbele ya Hakimu Aloyce Katemana.

Mshtakiwa huyo alisomewa shtaka hilo jipya na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, ambaye alidai Julai 3, mwaka jana katika kituo cha Polisi Oysterbay, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mulundi alitoa maelezo ya uongo kwa maofisa wa polisi, kwamba yeye pamoja na wenzake ambao hawapo mahakamani, walimtesa na kumteka nyara Dk. Ulimboka, taarifa ambazo siyo za kweli.

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka, na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika, na kuomba tarehe ya kutajwa pamoja na kusikiliza maelezo ya awali.

Wakili Kweka aliiambia Mahakama kuwa pamoja na kwamba dhamana kwa mshtakiwa iko wazi, Jamhuri inaomba Mahakama izuie dhamana kwa mshtakiwa huyo kwa sababu hana makazi maalum Tanzania na sababu za kiusalama kutokana na mazingira ya shauri hilo.

Alidai kwamba Mahakama ikimpa dhamana, itakuwa vigumu kwa mshtakiwa kujua tarehe ya kesi kwa sababu makazi yake hayajulikani.

Baada ya ombi hilo, mshtakiwa huyo alidai mahakamani hapo kuwa amekaa gerezani tangu mwaka jana; alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili na sasa amesomewa shtaka lingine.

“Sasa hivi wanasema nimetoa maelezo ya uongo, mheshimiwa wanataka kunipoteza nikiwa bado ni kijana mdogo, wanataka ku-silence (kunyamazisha), Bunge pamoja na wananchi,” alidai na kuongeza:

“Naumia kwa sababu nashtakiwa kwa kitu ambacho sikifahamu, mheshimiwa naenda kufanya demonstration (maandamano) na mgomo gerezani, nitachukua uamuzi ambao wewe mwenyewe utasikia.”

Hata hivyo, Mahakama ilisikiliza ombi la upande wa Jamhuri la kumnyima dhamana mshtakiwa na kurudishwa rumande hadi Agosti 20, mwaka huu.

Julai 13, mwaka jana Mhindi alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akiwa anakabiliwa na mashtaka mawili. Katika shitaka la kwanza, ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo Juni 26, mwaka jana, katika eneo la Leaders Club, alimteka Dk. Ulimboka.

Shitaka la pili, anadaiwa Juni 26 mwaka jana, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.

MBWEMBWE ZA POLISI BAADA YA KUMKAMATA
Julai 13, mwaka jana, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilimkamata Mhindi na kumfikisha Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashtaka ya utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleman Kova, alisema mtuhumiwa alikutwa na kitambulisho cha taifa la Kenya namba 29166938 kinachoonyesha kimetolewa Oktoba, 2010 Wilaya ya Nyeri.

Pia alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na hati ya kusafiria ya dharura namba 0123431 inayoonyesha imetolewa Juni 14, mwaka jana Namanga Arusha.

Alifafanua kuwa mtu huyo alifika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe, jijini Dar es Salaam ambalo kiongozi wake ni Mchungaji Joseph Gwajima na kutaka kuonana naye bila mafanikio.

Alisema mtuhumiwa huyo alifanikiwa kuonana na Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo, Joseph Kiriba na kumweleza kuwa yeye ni mwanachama wa kikundi cha Mafia ambacho hukodiwa kufanya matukio ya kihalifu nchini Kenya na nje ya mipaka.

Kamanda Kova alisema mtuhumiwa huyo alijieleza alikuja Tanzania na wenzake 12, kwa lengo la kumdhuru Dk. Ulimboka, baada ya kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina, lakini anaaminiwa ni mtumishi wa serikali.

Baada ya utekelezaji wa tukio hilo, wenzake waliondoka Dar es Salaam na yeye kwenda kanisani hapo kufanya toba.

Aliongeza kuwa kufuatia tukio hilo, raia wema walitoa taarifa polisi na kufanikisha kukamatwa kwa mshtakiwa huyo.

Kamanda Kova alisema katika mahojiano ya awali mtuhumiwa huyo alidai ni mwanachama wa kikundi cha kihalifu kinachojulikana kama Gun Star, kilichopo eneo la Ruiru Wilaya ya Thika nchini Kenya.

Alisema mtuhumiwa huyo alimtaja mmiliki wa kikundi hicho anayejulikana kwa jina la utani kama Silencer akisaidiana na Past, ambao wamemfundisha matumizi ya silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini humo.

Alisema mtuhumiwa huyo alidai kuwa kati ya watuhumiwa wenzake 12, aliwafahamu wawili tu ambao alisafiri nao kutoka mjini Moshi kuja Dar es Salaam kwa ajili kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka ili ataje wanaomtuma kushawishi mgomo wa madaktari nchini.

Mtuhumiwa huyo aliliambia Jeshi la Polisi kuwa waliambiwa baada ya kukamilisha kazi waliyotumwa, wamuue Dk. Ulimboka na waliahidiwa kulipwa fedha nyingi ambazo hakuzitaja.

Kamanda Kova alisema katika mahojiano zaidi na mtuhumiwa huyo, alibainisha kuwa, Juni 26, mwaka huu walisafiri kuja Dar es Salaam kwa basi asilolikumbuka na kukutana na mwenyeji ambaye alimpeleka hoteli moja iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Ilidaiwa siku hiyo baada ya kufika walipanga namna ya kutekeleza kazi waliyotumwa kuifanya usiku huo, na kwamba alishindwa kuondoka baada ya tukio kutokana na kuona kuwa kitendo alichokifanya ni cha kinyama na kuamua kukimbilia kanisani kwa toba.

Siku chache baada ya Kova kutoa taarifa hiyo, Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Josephat Gwajima, alikana kuwa mtu huyo alikwenda kutubu kanisani hapo.

Mchungaji Gwajima alisema makanisa yote ya watu waliookoka hayana utaratibu wa waumini kutubu kwa wachungaji.

Pia alisema mtu huyo baada ya kukamatwa, walinzi wa kanisa hilo walikubaliana na polisi wamwachie hasa baada ya yeye mwenyewe kueleza kuwa ana matatizo ya akili na hivyo amekuwa na tabia ya kuropoka ropoka hata katika mambo ambayo siyo ya kweli.

MAKINDA AZUIA MJADALA

Mwaka jana katika vikao vya Bunge, Spika Anne Makinda, alizuia mijadala ya baadhi ya wabunge waliotaka kuihoji serikali kuhusu kutekwa kwa Dk. Ulimboka kwa madai kuwa kulikuwa na kesi mahakamani.

Aidh, hatua hiyo ya kuachiwa mtuhumiwa huyo, inakuja wakati matukio ya kuteswa kwa Mhariri wa New Habari, Absalom Kibanda na mauaji ya Padre Evaristus Mushi, wa Kanisa Katoliki hajayapatiwa majibu yoyote mpaka sasa.

Aidha, uchunguzi wa matukio mawili ya milipuko ya mabomu mkoani Arusha nao haujapatiwa majibu licha ya Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi.

Tukio la kutekwa na kupigwa. Dk. Ulimboka, lilisababisha serikali kulifungia gazeti la Mwanahalisi kwa madai kuwa lilikuwa limeandika habari za uchochezi dhidi ya serikali, baada ya kutaja majina ya maofisa wa Usalama wa Taifa waliohusika na tukio hilo.


0 comments:

 

LIKE PAGE YETU UWE WA KWANZA KUPATA HABARI MPYA. Just Click Like Button Below...

Powered By OnlineBlogger