KANISA KATOLIKI PAROKIA YA URU LAKUMBWA NA MAMBO YA KISHIRIKINA....!!


HOFU kubwa imetawala Kanisa Katoliki Parokia ya Uru iliyopo Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, kutokana na matukio kadhaa yanayoendelea kutokea katika kanisa hilo huku baadhi ya watu wakiyahusisha na imani za kishirikina. 


  Katekista wa parokia hiyo, Lucian Tesha, aliwaambia waamini waliokusanyika katika ibada ya misa ya kwanza kanisani hapo juzi Jumapili kuwa usalama katika kanisa hilo upo shakani na kuwataka kuwa macho.


Hali hiyo inatokana na kile alichodai kuwa kuna mtu mmoja (mwanaume) kwamba amekuwa akionekana eneo la kanisa akiweka vitu mbalimbali ambavyo havina nia njema na kanisa hilo la Moyo Mtakatifu wa Yesu.
 
“Mtu huyu ameonekana kanisani hapa kwa mara ya nne sasa, hatujui anataka nini, lakini amekuwa akiweka vitu mbalimbali katika sanamu ya Bikira Maria na karibu na sakristi ya mapadri…kwa kweli hali hii inatisha.

 "Ninawaomba tunapotoka kanisani hapa tuende kuangalia katika sanamu hiyo, kwani mtajionea vitu hivyo na wakati mwingine hata kadi za pikipiki,” alisema Tesha na kuacha waamini wakinong’ona.


Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kanisani hapo ni kuwa tangu paroko mpya aingie katika parokia hiyo, aliyefahamika kwa jina moja la Kiondo kumekuwa na matukio ambayo si mazuri.


“Tangu aingie hapa sanamu ya Mtoto Yesu imeibiwa na watu wasiofahamika… hatujakaa vizuri yanajitokeza haya mauzauza ya watu kuweka vitu visivyofahamika kanisani.

“Haifahamiki kama wanampima au la, lakini wengi wanajiuliza ni kwa nini matukio haya hayakuwapo siku zote? Alihoji muumini mmoja.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya makanisa kushambuliwa na hivyo kuwaweka roho juu waamini na mapadri wanapokuwa wakishiriki ibada takatifu

0 comments:

 

LIKE PAGE YETU UWE WA KWANZA KUPATA HABARI MPYA. Just Click Like Button Below...

Powered By OnlineBlogger